August 6, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbolea ya fomi yaleta neema kwa wakulima

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Tabora

WAKULIMA wa zao la tumbaku na mazao mengine mkoani Tabora wametakiwa kuchangamkia mbolea ya Fomi inayozalishwa hapa nchini na kampuni ya Itracom Fertilizers Limited kwa kuwa inarutubisha udongo na kupata mavuno mengi zaidi.

Hayo yamebainishwa na Ofisa Mauzo wa kampuni hiyo mkoani hapa,Yusuph Said, alipokuwa akiongea na waandishi wa habari walipotembelea banda la kampuni hiyo kwenye viwanja vya maonesho ya Nanenane Ipuli,mkoani humo.

Ameeleza kuwa mbolea za Fomi tayari imeleta mageuzi kwa wakulima wa tumbaku na mazao mengine katika mikoa ya Kigoma na Tabora na maeneo mengine walioitumia msimu uliopita kutokana na virutubisho vilivyomo.

“Mbolea za Fomi ni mkombozi kwa wakulima, kwa kuwa zina mchanganyiko wa mbolea za asili yaani samadi na chokaa, na zimechanganywa na mbolea ya chumvi chumvi hivyo kuwezesha mkulima kupata matokeo chanya na ya haraka,”ameeleza.

Amesema mbolea hiyo huleta matokeo chanya na ya kudumu shambani,hivyo kumwezesha mkulima kupata mavuno mengi, kuvuna majani ya tumbaku yenye ubora wa daraja la juu ambayo yana bei nzuri sokoni.

“Katika msimu uliopita wakulima waliotumia mbolea hii kwenye kilimo cha tumbaku na mazao mengine walipata manufaa makubwa, hivyo natoa rai kwa wakulima wote kuchangamkia mbolea hizi ili wainuke kiuchumi,”.

Kwa upande wake Mohamed Luwanji (mkulima wa tumbaku na mahindi kutoka Kata ya Uyowa wilayani Kaliua mkoani Tabora amekiri kupata mavuno mengi zaidi ya tumbaku na mahindi baada ya kutumia mbolea hiyo tofauti na misimu ya nyuma.