Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
SERIKALI imesisitiza kuwa itaendelea kuunga mkono taasisi zinazowezesha maendeleo ya sekta ya kilimo, ikieleza kuwa sekta hiyo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa nchi na chanzo kikuu cha ajira kwa Watanzania wengi.
Kauli hiyo imetolewa leo na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Chande, alipotembelea banda la Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma.

Akiwa katika banda hilo, Chande alipata maelezo kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na TADB, ikiwemo mikopo kwa wakulima na wawekezaji wa sekta ya kilimo, pamoja na programu zinazolenga kuwawezesha vijana, wanawake na wajasiriamali wa kilimo.
Baada ya kupokea maelezo hayo, Naibu Waziri aliipongeza TADB kwa kuendelea kuchochea maendeleo ya sekta ya kilimo kupitia utoaji wa huduma za kifedha zinazowawezesha wakulima, wafugaji na wadau wengine wa mnyororo wa thamani kuongeza uzalishaji na tija. Alisema juhudi hizo zina mchango mkubwa katika kuimarisha usalama wa chakula, kuongeza kipato cha wananchi na kukuza uchumi wa taifa.

Maonesho ya Nanenane yanaendelea kuwa jukwaa muhimu kwa taasisi za umma na binafsi kuonesha teknolojia, huduma na fursa mbalimbali zinazochochea maendeleo ya sekta ya kilimo, huku TADB ikiwa miongoni mwa taasisi zinazotoa elimu na huduma za kifedha kwa wadau wa sekta hiyo.

More Stories
Ukaguzi wa migodi waimarisha Usalama,Uhifadhi wa Mazingira
CDICD yaongeza thamani ya madini Black Granite
Wahamasishwa kutumia mbegu bora za mifugo kuongeza tija