May 10, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Katibu mkuu Umoja wa Vijana (UVCCM) Taifa Raymond Mangwara akimkabidhi mbunge mteule wa Jimbo la Kigamboni Dkt.Faustine Ndungulile moja ya vitabu vya ilani ya chama cha mapinduzi katika viwanja vya Swala na wengine ni makada chama hicho.Mpigapicha Wetu

Ndungulile aahidi Kigamboni kuwa kituo cha uwekezaji

Na Bakari Lulela,TimesMajira Online, Dar

MGOMBEA ubunge kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Jimbo la Kigamboni Dkt.Faustine Ndungulile amesema kuwa endapo watamchagua Rais,mbunge na madiwani kupitia chama hicho watahakikisha kuwa wanaimarisha miundombinu ya barabara ikiwa ni pamoja na kumaliza tatizo la maji.

Akizungumza juzi kwenye mkutano wake wa kampeni amesema kuwa endapo watamchagua katika Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 28, mwaka huu, atahakikisha kuwa anawaletea maendeleo kwa kushirikiana na uongozi wa juu pamoja na wadhamini.

Katibu mkuu Umoja wa Vijana (UVCCM) Taifa Raymond Mangwara akimkabidhi mbunge mteule wa Jimbo la Kigamboni Dkt.Faustine Ndungulile moja ya vitabu vya ilani ya chama cha mapinduzi katika viwanja vya Swala na wengine ni makada chama hicho.Mpigapicha Wetu

Amesema atahakikisha zoezi la usambazaji wa maji safi na salama linakamika ambapo kwa sasa Serikali imeshatoa kiasi cha shilingi bilioni 12 kwa ajili ya usambazaji wa maji kwa wakazi wa wilaya ya Kigamboni.

Ndungulile amesema ataifanya Kigamboni kuwa kitovu cha uwekezaji kwa kuwa wameshatenga pamoja na kupima eneo la Pemba Mnazi kwa ajili ya ujenzi wa viwanda mbalimbali vyenye lengo la kuinua uchumi na kutoa ajira kwa vijana wa eneo hilo.

Aidha alieleza kuwa atakapo chaguliwa ataendelea kuboresha huduma za afya kwa kujenga vituo vya afya katika maeneo ya Kibada na Mwasonga ili wananchi wa maeneo hayo waweze kupata huduma rafiki kwa haraka sambamba na upatikanaji wa umeme wa kutosha.

Akitoa vipaumbele hivyo jijini Dar es Salaam katika viwanja vya swala wakati akiendeleza kampeni za kunadi sera zake kwa wananchi wa jimbo la Kigamboni kuomba kura kwa ajili ya kuendelea kuwaongoza katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

“Nawashukuru wananchi wa Kigamboni kwa kuniamini kwa miaka mitano iliyopita ambapo nimehudumu nafasi ya ubunge wa jimbo hili na sasa naomba kura zenu lakini pia niendelee kukishukuru chama changu kwa kuniamini kuendelea kuwatumikia wananchi wa Kigamboni kwa miaka mitano mingine,” amesema Dkt. Ndungulile

Dkt.Ndungulile ametumia fursa kuwaeleza kwa kifupi wananchi wa Kigamboni kile alichokuwa amekifanya katika kipindi cha miaka mitano ya Serikali ya Dkt. John Magufuli ni kuwa na wilaya inayoitwa Kigamboni pamoja na kujenga makao makuu ya wilaya hiyo ambapo mwaka 2015 haikuwepo.

Mgombea huyo amewaeleza wakazi hao kuwa wakielekea kwenye maeneo ya Somagila katika pori lililokuwa likimilikiwa na NAFCO wametenga hekari 715 kwa ajili ya maendeleo ambapo kwa sasa wamejenga majengo ya Halmashauri pamoja na jengo la mkuu wa mkoa wa Kigamboni alisema mahala hapo ndipo patakuwa pakifanyika shughuli za kiwilaya ikiwemo ujenzi hospitali, Soko, kituo cha daladala na kiwanja cha michezo.

Kuhusu sekta ya umeme Dkt.Ndungulile amesema alipoingia madarakani kulikuwa na mitaa 36 ambayo haikuwa na huduma hiyo ambapo amesema kwa sasa katika maeneo ya Kimbiji, Pemba mnazi, Kisarawe 2 na Somagira yamewekewa nguzo na kutandaziwa waya ili kuweza kukamilisha idadi ya jumla ya mitaa 67 ya wilaya hiyo.

Katika sekta ya miundo mbinu Dkt. Ndungulile amesema mwaka 2015 ujenzi wa daraja la Nyerere lilikuwa halijakamilika ambapo kwa sasa wameweza kulikamilisha sambamba na ujenzi wa barabara kutoka eneo hilo kwenda maeneo mengine, hata hivyo kwa upande wa Vivuko alieleza wanazaidi ya Vivuko vitatu ambavyo ni MV kazi, MV Magogoni na MV Kigamboni vyote vikiwa vinafanyakazi ya kuwahudumia wananchi.

Katika huduma za Kimahakama Mgombea huyo alisema alipoingia madarakani mwaka 2015 huduma hizo walizipata katika wilaya ya Temeke lakini hivi sasa Serikali ya Dkt.John Magufuli imejenga mahakama zipatazo mbili ikiwemo mahakama ya mwanzo na ya wilaya kwa ajili ya wakazi wa Kigamboni.

Kwa upande wa sekta ya afya alisema wameweza kuboresha vituo vya afya katika maeneo ya Kigamboni na kimbiji ambapo kwa wakati huu vinatoa za upasuaji kwa sasa zaidi ya akina mama wapatao 300 wameshapata huduma za uzazi sambamba na uwepo wa vitengo vitoavyo huduma za X-ray ndani ya vituo hivyo.

Kwa upande wake Katibu mkuu wa umoja wa vijana wa chama cha mapinduzi Taifa Raymond Mangwara aliwataka wakazi wa Kigamboni kuacha kusikiliza maneno yasiyokuwa na mashiko kutoka vyama vingine ila wawachague wagombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa nafasi ya Urais,Ubunge na Udiwani.

“Kigamboni itaendelea kung’ara zaidi kama wananchi mtawachagua wagombea wa Chama cha Mapinduzi kwa ngazi zote kwa kuwapiga kura za ndio hivyo ninawaomba kwa ridhaa yenu kujitokeza na kwa wingi kuchagua Serikali ya CCM.