April 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zimamoto wazingatie afya na utimamu

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Daniel Sillo (Mb) amewakumbusha Maofisa na Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuzingatia afya pamoja na kufanya mazoezi ya utimamu wa mwili kwa sababu kazi ya uokozi inahitaji nguvu na maarifa.

Sillo ameyasema hayo Aprili 16, 2024 wakati akizungumza na Maofisa na Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji alipotembelea Makao Makuu ya Jeshi hilo jijini Dodoma kwa ajili ya kujitambulisha na kufahamiana tangu kuapishwa kwake Aprili 4, 2024 na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

“Nimejifunza na kujua lengo kuu la kuanzishwa kwa Jeshi hili kuwa ni kuokoa maisha na mali za Watanzania na hata wasio Watanzania hivyo mzingatie sana na kuweka moyoni kwamba kazi yenu ni kuwahudumia Watanzania hivyo fanyeni kazi kifua mbele kwa kujitoa kuwahudumia kwa weledi na uzalendo,”amesema Sillo.

Sanjari na hayo amemuelekeza Kamishna Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji kuendelea kuboresha huduma kwa Wazimamoto na Waokoaji kwa kuongeza mikakati ya kuwapatia uwezo wa mafunzo na vifaa pamoja na msaada wa kisaikolojia kwani uwekezaji katika mafunzo kwao ni jambo la msingi na halipaswi kukwepwa.

Hata hivyo ametoa pole kwa Askari wote waliopata ajali ya kuungua moto wakati wakiwa katika harakati za kufanya uokozi kwenye ajali ya basi pamoja na lori la mafuta iliyotokea hivi karibuni eneo la Mlandizi mkoani Pwani.

Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji John Masunga, alimpongeza na kumshukuru Mhe. Sillo kwa kuonesha shauku ya kutaka kujua majukumu ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na changamoto zake.