May 2, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Jafo:Ukusanyaji chupa za plastiki ni lazima siyo hiyari

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

WAZIRI  wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo amesema  serikali  inaenda  kupiga marufuku  kabisa  kuonekana kwa chupa yeyote ya plastiki mtaani hasa za rangi  kwa kutengeneza kanuni  ambayo itakuwa  ni lazima mtu kukusanya chupa za kampuni yake.

Dkt Jafo amesema hayo jijini hapa  leo April 17,2024  katika kikao na wadau wanaozalisha bidhaa zinazofungashwa  kwenye chupa za plastiki na vifungashio vya plastiki   kwa lengo la kujadili njia bora ya kutokomeza  uchafuzi wa mazingira kwa kutumia vifungashio hivyo.

Amesema kuwa serikali inaenda kutekeleza hatua za mapitio ya kanuni za usimamizi wa taka ngumu za mwaka 2009 ambapo amesema jambo la ukusanyaji
wa chupa za rangi siyo la hiari tena ni jambo la lazima hivyo amewataka wadau hao peleka meseji kwa wazalishaji wenzeo ambao hawajahudhuria kikao hicho.

Amesema kuwa kutokana na michango mizuri ya wadau sasa wanaenda kutengeneza kanuni ambayo ndiyo itakwenda kutumika siyo tena kwa hiari mtu afanye anavyotaka yeye ambapo amesema kama nchi itakuwa imepiga hatua sana.

Kutokana na hayo ametoa maelekezo kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais kuhakikisha wataalamu kwa kushirikiana na wadau wanakamilisha kanuni hizo kabla ya Bunge la bajeti kuisha.

“Katika hili niagize ofisi yangu kupitia katibu mkuu hakikisheni nataka kuona kabla ya bunge la bajeti halijaisha kanuni iwe imeshatangazwa katika gazeti la serikali na wadau mkiwa na mawazo mengine ya ziada wataalamu wapo pelekeni mawazo ya ziada vipi kuboresha eneo hili,”amesema.

Vilevile ametoa maelekezo kwa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwamba baada ya kanuni  hiyo wakasimamie vizuri na  mzalishaji ambaye chupa yake itaonekana mtaani lazima aulizwe kwanini chupa yake ipo mtaani.

“Na hii hoja ya vifuniko ambayo Naibu Katibu mkuu amefusia hapa mkaifanyie kazi mkaangalie nini kifanyike hii mifuniko isonekane lengo kuhakikisha tunafika mahali pazuri .

“Tukitaka uwekezaji zaidi na mazingira yawe mazuri hivyo imani yangu mtajadili vizuri,vifungashio viwe vizuri,bidhaa ziuzike lakini kikubwa hapa ni kuzingatia kanuni hivyo makatibu wa kuu muandike kanuni mapema hadi wiki ijayo niwe nimeshiapata mchakato ufanyike kwenda kwenye utunzaji sahihi wa mazingira.

Hata hivyo amesema Ofisi yao imeweka utaratibu mzuri wakuona nini kifanyike na hata kwenye kanuni watajiwekea utaratibu mzuri.

“Ikiwezekana tufike wakati tuweke utaratibu leo tupo na wadau lakini ikiwezekana tuangalie Halmashauri wale ambao halmashauri zao chafu takataka zimejaa.

“Barabara nzuri lakini zimejaa takataka ikiwezekana tuwawekee kanuni katika zile zao ambazo wamejiwekea za kuzoa takataka pengine msimamizi hayupo vizuri,”amesema Dkt.Jafo.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira,Christina Mndeme ametoa wito kwa wadau hao kuangalia namna ya kutokomeza vifuniko vya chupa hizo kwnai nazo zimekuwa tatizo vimezagaa kila mahali.

“Muangalie na vifuniko vimezagaa kila mahali ni hatari hata kwa watoto wetu unaweza ukamkuta mtoto anakitafuna jambo ambalo ni hatari sana,”amesema.