September 1, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Yas yawashika mkono mama wajawazito Hospitali ya Ubungo

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira

WAJAWAZITO wanaopata huduma katika Hospitali ya Wilaya ya Ubungo, Dar es Salaam, watanufaika na vifaa vya kujifungulia pamoja na vifaa tiba vilivyotolewa na wafanyakazi wa Yas Tanzania katika jitihada za kumshika mkono akina mama wajawazito.

Msaada huo ulitolewa kupitia Kampeni ya Tumaini, ambao ni mpango ulioanzishwa na wafanyakazi wa Yas, umeanza na hospitali hiyo huku ukitarajiwa kuendelea katika maeneo mengine mbalimbali nchini.

Kupitia kampeni hiyo, Yas imekabidhi vifaa vya kujifungulia, khanga, vitanda vya uchunguzi kwa wajawazito, mashuka, aproni na viti mwendo.

Afisa Mkuu wa Rasilimali Watu wa Yas Tanzania, Caroline Kavishe, amesema kampeni hiyo ni wazo la wafanyakazi wa Yas ambao wameamua kutumia nguvu yao ya pamoja kufanya jambo lenye manufaa kwa jamii.

“Tumaini ni kampeni inayoendeshwa na wafanyakazi wetu. Wamechagua kusimama pamoja na akina mama wajawazito kwa kutambua ugumu wa nyakati ambazo wanapitia katika kumleta mtoto duniani.

“Tunataka wafanyakazi wetu wajivunie si tu kwa kazi wanayofanya, bali pia mchango chanya wanaoweza kuuleta katika jamii,” amesema Kavishe.

Kavishe amesema kampeni hiyo pia inatambua mchango mkubwa wa madaktari, wauguzi na watoa huduma wengine wa afya ambao kila siku wanahudumia wajawazito, akina mama na watoto wachanga.

Kwa upande wake Meneja wa Mahusiano ya Nje – Yas Tanzania, Rukia Mtingwa, alisema wazo la kampeni hiyo limetokana na kutambua umuhimu wa kusimama pamoja na akina mama katika kipindi muhimu cha ujauzito na kujifungua.

“Kila mama anayekwenda hospitali kujifungua anakwenda na tumaini la kujifungua salama, kumbeba mtoto wake mikononi na kurudi naye nyumbani.

“Tukajiuliza, katika safari hii muhimu ya mama na mtoto, sisi tunaweza kufanya nini? Ndiyo maana tumeunganisha nguvu zetu na kuanza hapa Ubungo,” amesema Mtingwa.

Akizungumzia dhamira ya Yas kwa jamii hivi karibuni, Mtingwa amesema kampuni inaangalia wajibu wake kwa upana zaidi ya kutoa huduma za mawasiliano na teknolojia.

“Tunaposema Mtandao wa Viwango, kwetu si suala la simu, intaneti na teknolojia pekee. Vilevile, ni suala la viwango vya namna tunavyowajibika kwa jamii. Tunataka popote Yas ilipo, jamii ihisi uwepo wetu kupitia mambo yanayogusa maisha yao,” amesema.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Ubungo, Dkt. Chrispin Kayola, amesema vifaa hivyo vitaongeza uwezo wa hospitali katika kuwahudumia wajawazito na akina mama wanaofika kujifungua.

“Tunapokea wajawazito karibia 150 kwa mwezi kipindi kama hiki cha low season na nusu kati yao huhitaji huduma za upasuaji, hivyo vifaa hivi vina umuhimu mkubwa sana kwa hospitali yetu. Vitasaidia kuwaongezea watoa huduma wetu nyenzo wanazohitaji kuwahudumia akina mama,” amesema Dkt. Kayola.

Kampeni ya Tumaini inatarajiwa kuendelea katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwapa wafanyakazi wa Yas nafasi ya kushiriki moja kwa moja katika kusaidia jamii, huku wajawazito na akina mama wakiwa miongoni mwa walengwa wa kampeni hiyo.