September 1, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Othman atoa wito malezi bora kujenga jamii salama

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online,Unguja

MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha ACT Wazalendo,Alhaj Othman Masoud Othman, usiku wa kuamkia,leo Septemba 01, 2026, alipata fursa ya kujumuika na waumini wenzake wa Kiislamu katika hafla ya Maulid iliyofanyika Nungwi – Kiungani, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Maulidi hayo ya kumbukizi ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W), ambayo hufanyika kila mwaka katika mwezi wa Mfunguo Sita, yaliandaliwa na wananchi wa kijiji cha Nungwi Kiungani.

Akitoa salamu zake kwa nyakati tofauti mbele ya mamia ya waumini waliojitokeza katika hafla hio, Alhaj Othman alikumbusha umuhimu wa kutoa malezi bora kwa watoto ili kujenga jamii iliyo salama.

“Dunia imekumbwa na wimbi la utandawazi ambao kama hatutowapa elimu na makuzi mazuri watoto wetu, basi dunia yao haitokuwa salama,”amekumbusha.

Amesisitiza kuwa jamii inapaswa kusimamia Qur’ani Tukufu, ambayo haina shaka ndani yake, ili kujiepusha na mikanganyiko ya baadhi ya wapotoshaji duniani.

Ameongeza kuwa mafunzo bora ya Kiislamu ni daraja la kupata viongozi waadilifu na raia wema, huku akiahidi kushirikiana na wananchi wa eneo hilo na Zanzibar kwa ujumla, kuleta maendeleo ya dini, ikiwemo kupigania uwepo wa Mfuko wa Zaka utakaokuwa kichocheo cha kusimamia mambo ya kheri.

Akitoa shukrani kwa niaba ya wananchi wa kijiji hicho, Bwana Hassan Jani Masoud, alisema kuwa hafla hiyo iliyojumuisha pia kundi kubwa la watoto wa Madrasa — ni kielelezo cha malezi na makuzi bora yaliyofundishwa na Mtume Muhammad (S.A.W).

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini, jamii na siasa, wakiwemo Imamu wa Msikiti wa Ijumaa wa Masjid Rahmaan, Maalim Simba Ali Sheha, Mwenyekiti wa Mkoa wa kichama Kaskazini A Unguja Mcha Rajab Haji na Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana Mkoa wa mkoa huo Nassor Madai.

Shughuli mbalimbali zilipamba hafla hiyo, zikiwemo visomo vya Qur’ani kutoka kwa wasomaji mbalimbali wa Zanzibar, milango ya Maulid, kaswida, mawaidha, na dhikri kutoka kwa makundi mbalimbali ya wanaume na kina mama.