Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online, Dodoma
MBUNGE wa Viti Maalum Devotha Daniel , ameiomba Serikali kuhakikisha mali mbalimbali za wananchi zinasajiliwa rasmi ili zitumike kama dhamana ya mikopo, akisema hatua hiyo itasaidia kupunguza migogoro ya kifamilia inayotokana na watu kukopa kwa siri kwa kutumia mali za pamoja.
Devotha amesema hayo Bungeni jijini Dodoma akiunga mkono Mswada wa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha, akieleza kuwa sheria hiyo inalenga kuongeza fursa za wananchi kupata mitaji na kuinua shughuli zao za kiuchumi.
Amesema mswada huo unatoa fursa kwa wananchi kutumia mali mbalimbali, zikiwemo magari, mashine na mazao, kama dhamana halali ya mikopo, badala ya kutegemea zaidi mali zenye hadhi ya kawaida ya dhamana, ikiwemo ardhi.
Kwa mujibu wa Devotha, mfumo huo unaweza kusaidia kupunguza migogoro ya kifamilia inayojitokeza pale mmoja wa wanafamilia anapotumia mali za pamoja kupata mkopo bila kuwepo kwa utaratibu rasmi wa usajili na matumizi ya mali hiyo kama dhamana.
Aidha, amesema kurahisishwa kwa usajili wa taasisi mpya za ukopeshaji kutasaidia kuongeza ushindani katika sekta hiyo na hatimaye kuchangia kushuka kwa gharama za mikopo.
Amesema fursa hiyo pia inaweza kuwawezesha wanawake, vijana na wafugaji kupata mitaji kwa kutumia mali walizonazo, jambo ambalo litasaidia kukuza shughuli zao za kiuchumi na kuchangia ongezeko la Pato la Taifa kupitia mifumo rasmi ya kifedha.
Hata hivyo, ameitaka Serikali kupunguza gharama za usajili pamoja na ukataji wa bima zinazohusiana na mali zinazotumika kama dhamana, ili wananchi wenye kipato cha chini waweze kumudu taratibu hizo.
ameishauri Serikali kutoa elimu ya mikopo na masuala ya fedha kuanzia ngazi za chini, akisema elimu hiyo itawasaidia wananchi kuelewa wajibu na masharti ya mikopo kabla ya kuingia katika mikataba ya ukopaji.

More Stories
Yas yawashika mkono mama wajawazito Hospitali ya Ubungo
Othman atoa wito malezi bora kujenga jamii salama
Muswada wa Sheria ya Mikopo wawasilishwa bungeni