April 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wizi wa mifugo washamiri Rukwa

Na Israel Mwaisaka,TimesMajira Online

KAMANDA wa Polisi mkoani Rukwa, William Mwampaghale amewataka wananchi mkoani humo kushirikiana na jeshi la polisi ili kutokomeza tatizo sugu la wizi wa mifugo mkoani humo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda huyo amesema kuwa, tatizo hilo bado ni changamoto kwa kuwa bado linaendelea na bahati mbaya hata baadhi ya watendaji wa serikali hawako makini na kusababisha changamoto hiyo kuendelea katika mkoa huo.

Amesema kuwa, katika kipindi cha mwaka huu kuanzia mwezi Januari mpaka hivi sasa jumla ya ng’ombe 79 waliibiwa katika maeneo mbalimbali na jeshi la polisi kwa kushirikiana na raia wema lilifanikiwa kuwakamata ng’ombe 59 waliokuwa wakisafirishwa baada ya kuibiwa.

“Tatizo hili bado ni changamoto kwani katika kipindi cha mwaka huu polisi wamefanikiwa kuwakamata ng’ombe 59 kati ya 79 walioibwa sehemu mbalimbali wakiwa wanasafirishwa kwa ajili ya kwenda kuuzwa, tena mbaya zaidi watuhumiwa wa wizi huo wamekutwa na vibali vya kusafirishia ng’ombe hao,”amesema.

Amesema kuwa, baadhi ya watendaji wa vijiji wamekuwa wakitoa vibali vya kusafirishia ng’ombe bila kujiridhisha kama kweli ng’ombe hao wamenunuliwa ki halali, wao wanachojali tu nikupata fedha ya Mapato inayolipwa na anayechukua kibali bila kujali ng’ombe hao kama wamepatikana kihalali kwani wengine ni wanakuwa ni wa wizi.

Aidha, amewataka wananchi wa mkoa wa Rukwa kulinda mali zao pia kushirikiana na polisi mara kwa mara pindi panapojitokeza changamoto yoyote kwani kwa ushirikiano huo utaimarisha usalama sambamba na kufanikiwa kuwadhibiti wahalifu mbalimbali katika mkoa wa Rukwa.