Na Mwandishi Wetu, TimesmajiraOline,Arusha
SERIKALI imeipongeza Benki ya CRDB kwa mkakati wake wa kuhamasisha uwekezaji nchini, hususan kwa vijana, kupitia elimu ya fedha, uwekezaji katika hisa na uwezeshaji wa kiuchumi unaolenga kujenga kizazi kipya cha wawekezaji wa Kitanzania.
Pongezi hizo zimetolewa leo Mei 15, 2026 na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar kwenye Semina ya Wanahisa wa Benki ya CRDB ikiwa ni utangulizi kwa Mkutano Mkuu wa 31 wa Wanahisa wa Benki hiyo utakaofanyika kesho Mei 16, 2026, pia katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) chini ya kaulimbiu ya Vijana na Uwekezaji kwenye Hisa.

“Benki ya CRDB imeendelea kuwa mfano wa taasisi inayochochea ushiriki wa wananchi katika umiliki wa uchumi kupitia uwekezaji kwenye masoko ya mitaji. Kaulimbiu ya mwaka huu imebeba ujumbe mkubwa wa kimkakati kwa Taifa letu. Vijana hawapaswi kuishia kutafuta ajira pekee, bali wanastahili kushiriki katika umiliki wa uchumi na fursa kupitia uwekezaji” amesema Balozi Omar.
Balozi Omar ameipongeza Benki ya CRDB kwa hatua yake ya kufungua Ofisi ya Uwakilishi Dubai, akieleza kuwa hatua hiyo imefungua ukurasa mpya wa historia katika sekta ya fedha nchini na kuiweka Tanzania katika jukwaa la kimataifa la fedha na uwekezaji.
“Hatua hii inaonyesha maono mapana, ujasiri wa taasisi na imani kubwa katika uwezo wa Watanzania kushindana kimataifa” ameongeza Balozi Omar.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Abdulmajid Nsekela ameahidi kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kuwawezesha vijana kupitia huduma za fedha, ubunifu, elimu ya uwekezaji na programu za maendeleo ya ujasiriamali.

Amesema kupitia CRDB Bank Foundation na programu ya IMBEJU, benki hiyo imefanikiwa kufikia maelfu ya vijana na biashara changa kwa kuwapatia mafunzo, mitaji na fursa za kukuza biashara zao.
“Tunaamini vijana wa leo si wateja tu wa benki yetu, bali ndio wawekezaji, wabunifu na viongozi wa uchumi wa kesho. Ndiyo maana tunataka wawe sehemu ya safari ya ukuaji wa taasisi yetu na uchumi wa Taifa” amesema Dkt. Nsekela.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Profesa Neema Mori amesema uwekezaji katika hisa ni moja ya njia muhimu za kujenga ustawi wa kifedha wa muda mrefu kwa vijana na familia za Kitanzania.
Profesa Mori amesema Benki ya CRDB ni ushahidi hai wa namna uwekezaji wa muda mrefu unavyoweza kubadilisha maisha ya watu, akibainisha kuwa wanahisa wengi waliowekeza miaka zaidi ya 30 iliyopita leo wanashuhudia matokeo ya maamuzi yao ya kimkakati.

“Leo hii tunajivunia kuona Benki ya CRDB ikiwa taasisi kubwa zaidi ya fedha nchini na moja ya taasisi kubwa za kifedha katika Afrika Mashariki na Kati. Ukuaji huu umeambatana na ongezeko kubwa la thamani ya uwekezaji wa wanahisa wetu” amesema Profesa Mori.
Profesa Mori ameeleza kuwa ndani ya miaka mitatu iliyopita, thamani ya hisa za benki hiyo imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 253, huku hisa zake zikiuzwa kwa wastani wa sh. 2,800 kutoka sh. 460 mwaka 2023.
Amesema Bodi ya Wakurugenzi inatarajia kuwasilisha pendekezo la gawio la sh. 90 kwa kila hisa kutokana na matokeo mazuri ya kifedha ya mwaka 2025, ikiwa ni ongezeko la asilimia 38 ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Profesa Mori pia amesisitiza umuhimu wa kujenga utamaduni wa uwekezaji mapema kwa vijana na familia, akihamasisha wazazi kuwawekezea watoto wao hisa kama sehemu ya kuwajengea msingi wa maisha ya kifedha ya baadaye.
Benki ya CRDB ni moja benki zinazoongoza katika ukanda wa Afrika Mashariki, inatoa huduma kwa wateja wadogo, wakati na wakubwa ikiwamo huduma kwa wateja binafsi, huduma za hazina, huduma za bima, mikopo ya biashara, kilimo na uwezeshaji kwa wajasiriamali wadogo.
Benki ya CRDB ndio benki ya kwanza nchini Tanzania kutambuliwa na kampuni ya kimataifa ya utafiti ya Moodys Investors Service kuwa moja kati ya benki 10 imara na salama Afrika katika uwekezaji. Moodys imeipa Benki ya CRDB daraja la uimara la B1 ambapo ni daraja la juu zaidi kupatikana kwa mabenki na taasisi za fedha katika ukanda wa jangwa la Sahara.

Benki ya CRDB imekuwa kiungo muhimu cha biashara katika nchi za Tanzania, Burundi, Kongo ya DRC, na Dubai, Falme za Kiarabu kwa kuwahudumia wateja zaidi ya milioni sita, na kupitia mtandao mpana wa matawi zaidi 260 nchini, zaidi ya CRDB Wakala 40,000, ATM 600, mashine za manunuzi (PoS) zaidi 4,500 na Kituo cha Huduma kwa Wateja kinachotoa huduma saa 24 kwa siku saba za wiki.
Semina hiyo ya wanahisa imewakutanisha viongozi wa Serikali, wanahisa, wataalamu wa masoko ya mitaji, vijana pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya fedha kwa lengo la kujadili nafasi ya vijana katika uwekezaji na mustakabali wa uchumi wa Taifa kupitia masoko ya mitaji.


More Stories
CCM yatoa salamu nzito kwa Samia-Butiama
TAKUKURU Kinondoni yaainisha mafanikio Januari_ Machi 2016
Serikali yafikisha Umeme Katika Migodi 289 ya Wachimbaji Wadogo