May 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Mwambe atoa mabati 190, saruji mifuko 260 Masasi

Na Mwandishi wetu, TimesMajira,Online Mtwara

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji na Mbunge wa Masasi, Geoffrey Mwambe ametoa mabati 190 na saruji mifuko 260) kwa ajili ya ujenzi wa choo cha walimu, nyumba ya mwalimu na ujenzi wa zahanati katika jimbo hilo.

Akizungumza katika ziara aliyoifanya katika vijiji vya Chipole na Machombe katika kata za Marika na Mumbaka jimboni Masasi, Mwambe amesema lengo la kutoa vitu hivyo ni kusaidia juhudi za Serikali katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wa maeneo hayo.

“Vifaa hivi ni sehemu ya mchango na juhudi za Serikali katika kutatua kero zinazowakabili ili kuboresha mazingira mazuri ya ustawi wa wananchi,” amesema Mwambe.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji na Mbunge wa Masasi, Geoffrey Mwambe, (kulia picha ya chini) akikabidhi mabati kwa ajili ya ujenzi wa choo cha walimu, nyumba ya mwalimu na ujenzi wa zahanati katika jimbo hilo. Pia katika hafla hiyo alikabidhi na saruji mifuko 260

Amesema katika mifuko 260 ya saruji, mifuko 100 itatumika katika ujenzi wa choo cha walimu wa shule ya msingi Chipole huku mifuko 160 itatumika katika ujenzi wa zahanati ya Machombe.

“Natambua changamoto ya ukosefu zahanati na ukosefu wa vyoo vya walimu, hivyo basi kwa hiki kidogo kilichopatikana kitatumika katika kuongezea nguvu kwenye uboreshaji wa ujenzi huu,”amesema.

Aidha Mbunge huyo amesema bati 30 alizozitoa ni sehamu ya ujenzi wa choo hicho cha walimu na kuahidi zingine 160 kuzitoa siku chache zijazo kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ya Machombe.

Katika hatua nyingine, Mwambe aliwahakikishia wananchi hao kuwa kuwa mamlaka ya maji ya RUWASA watakamilisha mradi wa maji utakowezesha upatikanaji wa maji ya uhakika jimboni hapo.

“Kwenye suala la maji tumefikia pazuri na hivi karibuni maji yatapatikana kwa urahisi na tayari watu wa RUWASA wamesafikia hatu nzuri kwenye kuukamilisha mradi huu,”amesema.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Mumbaka, Hamisi Nikwanya amemshukuru mbunge huyo kwa niaba ya wananchi wa jimbo hilo kwa jitihada zake za kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo.

“Kwa dhati kabisa kwa niaba ya wananchi wenzangu, napenda kuchukua fursa hii kukushukuru kwa namna ambavyo unashiriki kikamilifu kwenye kutatua changamoto na kero mbalimbali zinazatukabili,” amesema Nikwanya.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji na Mbunge wa Masasi, Geoffrey Mwambe,akizungumza na wananchi wa jimbo lake la Masasi.

Naye Hamisi Msusa, mkazi wa jimboni hapo amesema imani ya wakazi wengi ipo kwa mbunge huyo na Serikali katika kuwasaidia kutatua kero mbalimbali na kuleta maendeleo ya Masasi kwa ujumla.

“Imani yetu kwa Serikali ya awamu hii na kwako wewe mwakilishi wetu ni kubwa na matumaini yetu ni kuwa Masasi inapiga hatua kwenye maendeleo na kero zinatatuliwa kwa wakati”. Amesema Msusa.