May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TCU yafungua udahili kwa waombaji wa Shahada ya kwanza

Penina Malundo, TimesMajira Online

TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imefungua rasmi dirisha la kwanza la udahili kwa wanafunzi wa elimu ya juu (shahada ya kwanza) kwa mwaka wa masomo wa 2021/ 2022 huku ikianisha sifa zinazohitajika kwa wanafunzi kusoma katika vyuo vikuu mbali mbali nchini.

Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa amesema kufunguliwa kwa dirisha hilo kumekuja baada kutangazwa kwa matokeo ya kidato cha sita Julai 10,2021.

Profesa Kihampa amesema, Tume imefungua dirisha hilo leo(jana) badala ya Julai 15,2021 tarehe iliyokuwa imepangwa awali ambapo litakuwa wazi hadi Agosti 5,2021.

“Tume inawahimiza waombaji wote wa udahili kuendelea kupata taarifa sahihi kupitia tofauti ya TCU,tovuti za vyuovilivyoruhusiwa kudahili wanafunxi wa mshahara za kwanza pamoja na taarifa mbalimbali zinazotolewa na TCU kupitia vyombo vya habari,”.

Udahili wa kujiunga na shahada ya kwanza utahusu waombaji waliohitimu wa kidato cha sita; wenye Stashahada (Ordinary Diploma); na waliomaliza programu ya ‘Foundation’ ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT).

Prof.Kihampa amesema ili kufahamu sifa stahiki za kujiunga na Chuo Kikuu waombaji wameelekezwa kusoma vigezo vilivyopo kwenye vitabu vya muongozo vya TCU huku pia wakitakiwa kutuma maombi yao moja kwa moja kwenye vyuo ambavyo wamevichagua na kwamba maelekezo ya jinsi ya kutuma maombi yanayotolewa na vyuo vikuu husika.

“Tunawaasa wananchi kuepuka kupotoshwa na watu wanaojiita mawakala au washauri wanaodai wanatoa huduma ya jinsi ya kujiunga na vyuo vya elimu ya juu hapa nchini kwani masuala muhimu ambayo waombaji wanapaswa kuzingatia ni pamoja na kusoma muongozo wa udahili na kuuelewa, kuingi kwenye tovuti za vyuo ili kujua taratibu za kutuma maombi, kutuma maombi moja kwa moja vyuoni kupitia mifumo ya kielektoniki na kuwasiliana na vyuo ili kupata taarifa,”.