Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
DIWANI wa Kata ya Nyamanoro wilayani Ilemela mkoani Mwanza,Abdulrahman Kange ameendelea kuunga mkono juhudi za wananchi wa Mtaa wa Nyamanoro Mashariki za kujenga barabara ya Sinza-Mjimwema kwa kiwango cha zege yenye urefu wa mita 500 kwa kutoa mifuko 10 ya saruji pamoja na kushiriki ujenzi wa barabara hiyo unaoendelea.
Akizungumza Agosti 15,2026 mara baada ya kukabidhi mifuko hiyo kwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyamanoro Mashariki Missa Budundu,Kange amewapongeza wananchi wa mtaa huo kwa kujitolea kurekebisha na kujenga barabara hiyo kwa kuchangia mfuko mmoja mmoja wa saruji kwa kila kaya.

“Kwa ushirikiano huo kati ya wananchi na viongozi,naamini muda si mrefu barabara hii itafika mwisho ili iweze kupitika vizuri na kusaidia vijana wetu,wanawake wanauza samaki na watu mbalimbali hasa wenye ulemavu waweze kupitia vyema.Hivyo leo nimetoka mifuko10,huu ni mwanzo nitaendelea kuwashika mkono ili kuhakikisha barabara yetu inakamilika,”amesema Kange.
Kange amesema, barabara hiyo hadi sasa inahitaji mifuko ya saruji 480 pamoja na mahitaji mengine ikiwemo mchanga na kokoto,hivyo ametoa wito kwa wadau na wananchi kuendelea kuchangia ili barabara hiyo iweze kupitika huku ujenzi ukiwa umefikia asilimia 45,hivyo matarajio yao kupitia michango ya wananchi na wadau ifikapo Desemba 2026,wanatarajia kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo.
Pia amesema,barabara hiyo inaunganisha kata hiyo na kata jirani,na ni kiungo ambacho siyo tu kinasaidia wakazi wa Nyamanoro pekee pia wakazi wa mitaa na kata jirani pamoja na kusaidia watu kufanya shughuli zao za maendeleo na kujipatia kipato.
Hivyo ametoa wito kwa viongozi wa Serikali za Mitaa na Halmshauri kuunga mkono jitihada ambazo wananchi wa mtaa huo wamezionesha ili kuhakikisha ujenzi wa barabara hiyo inakamilika na kutoa huduma kwa jamii.
“Sisi wananchi wa Kata ya Nyamanoro tumeanza lakini tunahitaji Serikali itushike mkono kuhakikisha kwamba tunakamilisha ujenzi wa barabara hii,”amesema Kange.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyamanoro Mashariki Missa Budundu amesema,mtaa huo umepokea mifuko 15 ya saruji kutoka kwa Diwani huyo kwa ajili ya ujenzi wa barabara ambapo awali alitoa mifuko mitano na leo mifuko 10.
Amesema,ujenzi wa barabara hiyo ulianza mwaka 2024 mara baada ya kuingia madarakani kwa nafasi ya Unyekiti,na mpaka sasa wameisha jenga urefu wa mita 100 kati ya mita 500 kwa nguvu za wananchi na wadau.Hivyo amewasisitiza wananchi wa mtaa huo kutekeleza walichokubaliana kwa kila mmoja kuchangia ujenzi kwa kila kaya kutoa mfuko mmoja wa saruji
“Bado mita 400 kukamilisha ujenzi wa barabara hii,na kila mita 25 tunatumia mifuko 30 ya saruji,hivyo bado tunahitaji mifuko 480 ya saruji,mchanga na kokoto,kwani barabara hii ni kiungo muhimu katika mitaa ya Nyamanoro na Kata jirani,”amesema Budundu.

Mmoja wa wananchi wa Mtaa wa Nyamanoro Mashariki Haruna Hamad amesema,ubovu wa barabara hiyo inawapa changamoto waendasha bodaboda na bajaji hasa kufikisha abiria,hivyo ikikamilika itarahisisha usafiri kwa wananchi huku Anastasia David amesema,barabara hiyo ni changamoto hasa kwa wajawazito pindi wanapotaka kwenda hospitali kujifungua.
Kwa upande wake Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Nyamanoro Mashariki Kezia Manyama amesema,kutokana na ubovu wa barabara hiyo umesababisha watu kujifungua njiani hivyo wanaposhirikiana wanatoa kitu kizuri.
“Ombi langu Serikali ituangalie kwa machi mawili,maana mtaa huu kuna wengine hawana kitu hivyo kufanya ujenzi unakuwa changamoto na wakati mwingine kushindwa kukamilisha,”amesema Manyama.


More Stories
Uwekezaji mkubwa katika elimu wamkosha mkuu wa shule ya sekondari Mkole
Jaji Mshibe asisitiza maandalizi ya Kisekta katika kukabiliana na athari za El Nino
Wki ya Elimu kuibu vipaji ,wabunifu