Na Joyce Kasiki, Geita
MKOA wa Geita unaendelea kunufaika moja kwa moja na uwekezaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kupitia Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) na kituo cha mafuta cha TANOIL kinachohudumia sekta ya madini na usafirishaji.
Akizungumza na waandishi Afisa Masoko wa TPDC, Grace Chigugu katika Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoani Geita.
Amesema ushiriki wa shirika hilo kwenye maonesho hayo unalenga kuwaonyesha wananchi na wadau jinsi miradi hiyo inavyochochea uchumi wa mkoa na fursa zinazofunguka kwa wafanyabiashara wa ndani.
Amesema TPDC kupitia kampuni tanzu ya TANOIL inamiliki na kuendesha kituo cha mafuta mkoani Geita ambacho kimekuwa mhimili muhimu wa nishati kwa shughuli za uchimbaji na usafirishaji wa madini.
Kuhusu EACOP, Grace amesema bomba hilo linalopita katika maeneo mbalimbali nchini limefungua fursa za ajira, huduma na biashara kwa wananchi wa Geita na mikoa jirani.
Sambamba na miradi hiyo, amesema TPDC inatoa elimu kuhusu majukumu yake ya msingi kuanzia utafiti na utafutaji wa mafuta na gesi, uzalishaji, uchakataji hadi usambazaji, pamoja na teknolojia za kisasa za utambuzi wa miamba yenye viashiria vya mafuta na gesi.
Katika banda la TPDC, wageni wanapata fursa ya kipekee ya kujionea teknolojia ya Ukweli Uhalisia (Virtual Reality) inayowawezesha kushuhudia kwa karibu namna miradi ya uchorongaji na usafirishaji wa gesi asilia inavyotekelezwa bila kufika eneo la mradi.
“Kupitia teknolojia hii wananchi wanapata uelewa wa kina kuhusu shughuli za mafuta na gesi kwa njia rahisi na ya vitendo,” amesema Grace.
Ameongeza kuwa Serikali ina mpango kabambe wa kusambaza gesi asilia katika mikoa ya kanda ya kaskazini na kati ikiwemo Morogoro, Dodoma, Tanga, Kilimanjaro na Arusha, huku Geita ikiwa miongoni mwa mikoa itakayonufaika katika miaka ijayo.
“Lengo ni kuhakikisha wananchi na viwanda vinapata nishati ya uhakika kwa gharama nafuu na kuchochea uzalishaji na uwekezaji nchini,” amesema.
TPDC imewataka wananchi na wadau wa madini kutembelea banda lake ili kupata elimu zaidi kuhusu huduma, teknolojia na fursa za uwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi.

More Stories
Serikali yaombwa kuweka utaratibu kutatua migogoro wachimbaji wadogo
Wakina mama wahimizwa kufanya mazoezi
ETDCO yawataka wachimbaji kutumia miundombinu yao