May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Naibu waziri asisitiza elimu ya mawasiliano

Penina Malundo

NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe , amesisitiza juu ya umuhimu wa wananchi kupata elimu stahiki juu ya matumizi sahihi ya huduma za mawasiliano.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati alipotembelea banda la maonesho la Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), katika viwanja vya Maonesho ya Biashara ya Kimataifa, yaliyomalizika jana jijini Dar es Salaam, Kigahe amesisitiza kuwa ni muhimu wananchi wakapata elimu ambayo inatolewa na Mamlaka hiyo juu ya matumizi sahihi ya huduma za mawasiliano.

Kigahe amesisitiza kuwa ili kutokomeza matukio ya utapeli mtandaoni wananchi hawana budi kushirikiana na Mamlaka hiyo katika kutoa taarifa juu ya matukio ya kitapeli kwenye mtandao, ikiwemo jumbe fupi za kitapeli zinazotumwa kwa watumiaji huduma za mawasiliano ili kuwalaghai.

Mamlaka ya Mawasiliano ilitoa namba maalum ambayo inamwezesha mtumiaji huduma za Mawasiliano ya simu kutoa taarifa juu ya ujumbe wowote wa kitapeli kwa kuutuma ujumbe huo kwenda namba 15040 ukihusisha namba ya mhusika anayefanya jaribio la utapeli kwa mtumiaji wa huduma za Mawasiliano.

Akiwa kwenye banda hilo Naibu Waziri aidha alipokea maelezo juu ya zoezi la uhakiki wa usajili wa laini za simu kwa mtumiaji huduma za Mawasiliano kwa kutumia namba maalum ya *106# inayomwezesha mtumiaji simu ya mkononi kupata maelekezo ya namna ya kuhakiki namba zilizosajiliwa kwa utambulisho wa namba za kitambulisho cha Taifa na ikiwa kuna namba ambazo mtumiaji hazitambui anapaswa kuzifuta kupitia kwa wakala wa usajili wa simu anayewakilisha kampuni husika ya Mawasiliano.

“Kwa mfano hata mimi laini yangu nimerudia yaani kwenda kuhakiki na kuhakiki tena, tunategemea zile namba za utapeli zisiwe zinatumika tena” amesema Kigahe.

Kigahe ameipongeza TCRA kwa kazi nzuri inayofanya ya kuelimisha umma juu ya matumizi salama ya huduma za Mawasiliano.

Maonesho ya 45 ya biashara ya kimataifa maarufu kama SabaSaba huwakutanisha wafanyabiashara na wajasiriamali mbalimbali wa kitaifa na kimataifa sambamba na taasisi ambazo hupata nafasi ya kuonesha bidhaa na huduma wanazotoa kwa jamii