May 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Mkuu Mstaafu wa Ethiopia asema Tanzania inaweza kulisha Afrika

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online. Bagamoyo

MWENYEKITI wa Bodi ya AGRA, Waziri Mkuu Mstaafu wa Ethiopia, Hailemariam Dessalegn, amesema Tanzania inaweza kuilisha Afrika iwapo mapinduzi ya kilimo yatafanyika kwa umakini na kwa ukamilifu.

Akizungumza baada ya kukagua kiwanda cha kusaga mahindi kinachomilikiwa na Kampuni ya Joydons Tanzania Limited akifuatana na Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete jana wilayani Bagamoyo, Dessalegn ameelezea kuridhishwa na uwekezaji uliofanywa na kiwanda hicho.

“Nimevutiwa na uwekezaji uliofanywa katika kiwanda hiki. Tanzania inaweza kulisha nchi za Afrika endapo mapinduzi katika sekta ya kilimo, mifuogo na uvuvi yatafanyika kikamilifu.

Kiwanda hiki ni kielelezo cha mapinduzi hayo kwa sababu kinaogeza thamani kwenye mazao ya kilimo. Kiwanda hiki kitasaidia kuhamasisha kilimo bora katika ukanda huu,” amesisitiza Dessalegn.

Benki ya Kilimo Tanzania (TADB) na Alliance for a Green Revolution in Africa (AGRA) wanashirikiana katika kuimarisha kiwanda hicho ambacho tayari kinanunua mahindi kutoka kwa wakulima wa Mikoa ya Pwani na Tanga na kuzalisha tani 150 za unga wa mahindi na kuusambaza mikoa mbalimbali ya Tanzania.

TADB imetoa mkopo wa sh.bil 1.2 kukiboresha kiwanda hicho.

7512
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo Tanzania (TADB) Derick Rugemala (kulia) akitoa maelezo kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Kimataifa ya Mapinduzi ya Kijani Africa(AGRA), Hailemariam Dessalegn (wapili kushoto) ambaye pia alikuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia alipotembelea kiwanda cha kuchakata mahindi cha Joydons Tanzania Ltd kilichopo Bagamoyo Mkoani Pwani ambacho kimepata mkopo wa sh. bilioni 1.2 kutoka TADB kwa kushirikana na AGRA. Kushoto ni Mjumbe wa Bodi ya AGRA na Rais Mstaafu wa Awamu ya nne,Dkt.Jakaya Kikwete.

Mwenyekiti wa Bodi ya TADB, Ishmael Kasekwa, ameueleza ugeni huo kwamba ushirikiano kati ya TADB na AGRA umekuwa na mafanikio makubwa na kwamba wanatumaini ushirikiano huo utaweza kuibua mageuzi yanayowaniwa katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.

“Benki yetu itaendelea kutoa mikopo ili kutekeleza azma ya Serikali ya kujenga uchumi wa viwanda inafikiwa kupitia kilimo.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TADB, Derick Rugemala, amesema ushirikano kati ya taasisi hizo mbili umetokana na uhitaji mkubwa uliopo kutosheleza mahitaji ya wadau wa kilimo.

“Kumekuwepo upotevu mkubwa wa mazao baada ya mavuno kwa sababu ya kukosa viwanda vya kuchaka mazao.

Hivyo tumeingia ubia huu wa kuiwezesha kampuni hii inayomilikiwa na wanawake wawili ili kiwanda kiweze kupunguza upotevu wa mazao,” amesema Rugemala na kueleza kwamba kumsaidia mwanamke ni kuisaidia jamii nzima na kwamba jambo hilo lilifikiriwa kwa makini na TADB na AGRA katika kuiwezesha kampuni ya Joydons ili nayo ihakikishe mahindi yanakuwa na soko la uhakika.

Amesema TADB inaendelea kupokea maombi ya mikopo kutoka kwa wadau kwenye mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi na kuyapima ili waombaji watakaopata mikopo wajikite kwenye uzalishaji wenye tija kuifanya Tanzania kujitosheleza kwa chakula na kuuza chakula nje.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Joydons Tanzania Ltd, Joyce Kimaro, ameishukuru TADB na AGRA kwa uwekezaji katika kiwanda chao na kueleza matarajio yake katika kuwafikia wakulima wengi na kununua mahindi yao kama malighafi ya kiwanda chao.

Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha Joydons T.Ltd, Joyce Donati Kimaro (Wapili kushoto) akitoa maelezo ya kiwanda chake alipotembelewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Kimataifa ya Mapinduzi ya Kijani Africa(AGRA), Hailemariam Dessalegn(kushoto) alipotembelea kiwanda hicho mara baada kukiwezesha mkopo wa bilioni 1.2 kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Nchini(TADB). Kulia ni Mjumbe wa Bodi ya AGRA na Rais Mstaafu wa Awamu ya nne,Dkt.Jakaya Kikwete. Wapili Kushoto ni Mkurugenzi Mwenza wa Kiwanda hicho, Joyce Donald Kimaro.

“Mpaka sasa tumewafikia wakulima zaidi ya 1,500 katika Mkoa wa Pwani na Tanga na ambapo tunachakata zaidi ya tani 150 ya mahindi kwa siku na kuyaongezea thamani kwa kuzalisha unga ambao tunauuza katika mikoa mbalimbali chini,” amesema Bi.Kimaro