May 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bilioni 1.2/- yatolewa kuendeleza kiwanda Bagamoyo

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online Bagamoyo

KAMPUNI ya Joydons T.Limited inayojihusisha na uchakataji wa mazao ya mahindi iliyopo Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani kimepata mkopo wa sh. bilioni 1.2 kutoka Benki ya Maendeleo ya kilimo (TADB) kwa kushirikiana na Taasisi ya kimataifa ya Mapinduzi ya Kijani Africa (AGRA) kwa lengo la kuongezea uwezo wa uzalishaji wa bidhaa zitokanazo na mazao ya mahindi.

Akizungumza mara baada ya ziara ya Mwenyekiti wa Bodi ya AGRA, Hailemariam Dessalegn ambaye pia alikuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia aliyeambatana na Rais Mstaafu wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete ambaye ni mjumbe wa bodi hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TADB, Derick Rugemala amesema ushirikano huu umetokana na uhitaji mkubwa uliopo kwa wadau wa kilimo.

“Kumekuwa na upotevu mkubwa wa mazao kutokana na kukosa viwanda vya kuchaka mazao hao hivyo tumeingia ubiwa na ukiweza kampuni hii inayomilikiwa na wanawake ili iweze kusaidia kuondoa upotevu wa mazao kwa kufanya uwekezaji wa kiwanda hapa Bagamoyo,” amesema Rugimala

Ameeleza kuwa ukimsaidia Mwanamke ni kwamba umeisaidia jamii nzima, hivyo TADB kwa kushirikana na AGRA imeiwezesha kampuni ya Joydons ili iweze kuifikia jamii kwa upana wake kwa kuhakikisha mazao ya mahindi yanakuwa na soko la uhakika.

“Tuna imani kuwa uwepo wa kiwanda hiki hapa Bagamoyo kutasaidia wakulima wa mikoa jirani kuwa na soko la uhakika la mazao yao na kupelekea uchumi katika maeneo haya kuongezeka,” amesema Rugimala

Ameeleza kuwa TADB inaendelea kupokea maombi ya mikopo kutoka kwa wadau kwenye mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kuzafanya uzalishaji wenye tija ambao utaifanya nchi yetu kujitosheleza kwa chakula na kuuza nje ya nchi.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo Tanzania (TADB) Derick Rugemala (kulia) akitoa maelezo kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Kimataifa ya Mapinduzi ya Kijani Africa(AGRA), Hailemariam Dessalegn (wapili kushoto) ambaye pia alikuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia alipotembelea kiwanda cha kuchakata mahindi cha Joydons Tanzania Ltd kilichopo Bagamoyo Mkoani Pwani ambacho kimepata mkopo wa sh. bilioni 1.2 kutoka TADB kwa kushirikana na AGRA. Kushoto ni Mjumbe wa Bodi ya AGRA na Rais Mstaafu wa Awamu ya nne,Dkt.Jakaya Kikwete.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya AGRA, Hailemariam Dessalegn amesema amevutiwa na uwekezaji uliofanywa na kiwanda cha Joydons na kwamba kitasaidia katika kuhamasisha kilimo bora kwa ukanda huu.

“Tanzania inaweza kulisha nchi za Afrika endapo mapinduzi ya katika sekta ya kilimo, mifuogo na uvuvi ikifanyika kikamilifu, alisema Bw.Dessalegn na kukitaja kiwanda cha Joydons kuwa kielelezo cha mapinduzi hayo katika kuongezea thamani mazao ya kilimo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Joydons Tanzania Ltd, Joyce Donati Kimaro ameishukuru TADB na AGRA kwa kumuweza kufanya uwekezaji wa kiwanda hicho na kueleza matarajio yake katika kuwafikia wakulima wengi kwa kununua mazao yao kama malighafi katika kiwanda.

“Mpaka sasa tumeweza kuwafikia wakulima zaidi ya 1,500 katika Mkoa wa Pwani na Tanga ambapo kwa siku tunachakata Zaidi ya tani 150 ya mahindi na kuyaongezea thamani kwa kuzalisha unga ambao tumekuwa tukiuza katika mikoa mbalimbali chini,” alisema Bi.Kimaro

Mwenyekiti wa Bodi wa TADB, Ishmael Kasekwa amesema ushirikiano kati ya TADB na AGRA umekuwa na mafanikio makubwa ambayo yanawezesha mageuzi katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi, hivyo Benki hiyo itaendelea kutoa mikopo ili kutekeleza azma ya Serikali ya kujenga uchumi wa viwanda inafikiwa kupitia kilimo.