April 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Dkt. Ndumbaro asitisha zuio usafirishaji nje bidhaa ghafi za misitu

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online Dar

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro amaondoa zuio la usafirishaji bidhaa ghafi za misitu kwa masharti ikiwemo ‘veener’ na utomvu kutoka miti ya misindano kwenda nje ya nchi mpaka Juni, 2022.

Aidha ameruhusu kontena 187 zilizopo bandari kusafirishwa na kontena zilizopo nje ya bandari zifuate utaratibu uliowekwa na Wizara ili zipate kibali cha kusafirishwa.

Akizungumza kwenye kikao kilichoratibiwa na Baraza la Biashara la Taifa (TNBC) Jijini Dar es Salaam, Dkt. Ndumbaro amesema lengo la Serikali ya Awamu ya Sita ni kuona sekta ya misitu inatoa mchango stahiki kwenye pato la taifa na kuwataka wadau kujiandaa na utekelezaji wa maazimio yaliyopitishwa kwenye kikao kilichowakutanisha wadau hao Novemba 15, mwaka huu Wilayani Mafinga.

“Malengo ya Serikali ni kuona sekta ya misitu inaleta tija kwa wazalishaji wake. Nyinyi kama wadau hamna budi kujiandaa kutekeleza maagizo ya serikali ambayo na ndiyo maana nimetoa zuio nililoliweka ili mupate muda wa kujiandaa,” alisema Dkt. Ndumbaro.

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Damas Ndumbaro, Akizungumza kwenye mkutano na wadau wa misitu ulioratibiwa na Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) uliofanyika Jijini Dar es salaam, lengo ni kujadili athari za katazo Serikali la usafirishaji wa bidhaa ghafi za misitu lilitolewa kwenye Kongamano la uwekezaji kwenye sekta ya misitu lililofanyika wilayani Mafinga Novemba 15, mwaka huu. Katika mkutano huo Waziri alitoa ruhusa ya kusafirisha wa mazao ya misitu aina ya Veneer mpaka juni 2022 kwa masharti yaliyowekwa na wizara.

Dkt. Ndumbaro amesisitiza kuwa; “Katika kipindi hiki cha mpito mpaka kufikia Juni mwakani vibali vyote vitatolewa na Waziri kwa kufuata masharti yakiwemo kuleta taarifa za kodi, taarifa za haki za wafanyakazi, thamani halisi ya mzigo pamoja na kuwa na mpango kazi wa kampuni wa kuleta mashine haraka.

Aidha, Dkt.Ndumbaro amewataka wafanyabiashara na Watanzania kwa ujumla kukubaliana na mabadiliko ambayo ndiyo msingi wa maendeleo katika jamii yoyote duniani hivyo amehimiza jamii kuwa katika mtazamo chanya katika kupokea mabadiliko.

“Serikali imefanya tafiti na kujiridhisha kuwa faida inayopatikana katika kusafirisha malighafi ni ndogo hivyo ili kukuza kipato kupitia sekta ya misitu imeamua kuzuia usafirishaji wa mazao hayo na kuhimiza uwekazaji utakaotoa bidhaa ya mwisho na kwenda sokoni,’’ amesema Dkt.Ndumbaro.

Aliongezea kuwa Serikali itaendelea kupaanua wigo na kutoa fursa zaidi za uwekezaji na ajira nchini kwani kwa kufanya zuio hilo kutachochea uwekezaji wa viwanda vikubwa hapa nchini jambo litakalozalisha ajira na kukuza pato la taifa.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa TNBC Dkt. Godwill Wanga mbali ya kumshukuru Waziri kwa kuja kuzungumza na wadau wa misitu, amewataka wadau hao kuwa na imani na Serikali, kwani imefanya maboresho hayo ili sekta hiyo iwe na tija kwa wazalishaji na kuchangia kwenye pato la taifa.

“Kwa muda mrefu sasa sekta ya misitu imeonekana ikitoa mchango mdogo kwenye pato la taifa, kwa kuliona hilo Serikali imekuja na maazimio haya ikiwa ni hatua ya kuifanya sekta hii iwe na tija sio tu kwa wazalishaji bali hata kwa uchumi wa nchi,” amesema Dkt. Wanga.

Dkt. Wanga ameongeza kuwa, “Sekta hii inahitaji tafiti nyingi ili wadau wajue fursa nyingi zaidi zilizopo, ambazo tukizutumia vyema itakuwa lulu kwa taifa.’’

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Damas Ndumbaro(katikati) akimsikiliza Mdau na mtengenezaji wa bidhaa zinazotokana na mazao ya misitu, Benson Maduhu (wapili kushoto) juu ya bidhaa anazotengeneza nchini kwenye mkutano na wadau wa misitu ulioratibiwa na Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) uliofanyika Jijini Dar es salaam, katika kujadili utekelezaji wa maazimio yaliyopitishwa kwenye kikao kilichowakutanisha wadau hao tarehe 15 mwezi huu wilayani Mafinga. Kulia ni Katibu Mtendaji wa TNBC, Dkt.Godwill Wanga na kushoto ni Mwenyekiti Mwenza wa kikundi kazi cha Misitu, Ben Sulus

Naye Mwenyekiti Mwenza wa kikundi kazi cha Misitu TNBC, Ben Sulus mbali ya kumpongeza Dkt. Ndumbaro kwa kutenga muda kuja kuwasikiliza wadau hao, aliwataka wadau hao kubadilika na kuendana na matakwa ya Serikali kwa kuwekeza zaidi kwenye kuleta mitambo na kuanzisha viwanda vingi nchini ili uzalishaji ufanyike hapa hapa jambo ambalo litatengeneza fursa kubwa za ajira kwa Watanzania.

“Sisi kama sekta binanfsi tujipange vizuri kwa kujiandaa kutekeleza kipindi hiki mpaka kufikia mwakani, tuweze kuanzisha viwanda vingi nchini vitakavyozalisha ajira kwa vijana wetu wengi zaidi”, alisema Bw. Sulus.

Waziri Dkt. Ndumbaro ameahidi kukutana tena na wadau wa sekta ya misitu Desemba 13 na 14 mwaka huu Jijini Arusha ili kuzungumza nao sambamba kuangalia namna utekelezaji wa maagizo ya Serikali unavyofanyika.