April 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ndugai awang’ata sikio wafanyabiashara nchini

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online Dodoma

SPIKA wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amewataka wafanyabiashara nchni kujenga tabia ya uaminifu kwenye shughuli zao kama kigezo pekee kitakacho wajengea imani kwa Serikali na jamii ili kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi.

Akizungumza kwenye hafla fupi iliyoandaliwa na Chemba ya Wafanyabiashara, wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) Jijini Dodoma jana,Spika Ndugai alisema Serikali inataka kuona sekta binafsi imara na inayokua, lakini inazingatia uaminifu na uwazi katika shughuli zake.

“Sisi kama Bunge tuna imani kubwa Serikali inapenda kuona sekta binafsi inakua na kutoa mchango stahiki katika maendeleo ya taifa.

Lakini kitu pekee ambacho tunategemea kuona kutoka sekta binafsi ni kuonesha uaminifu na kuwa wawazi katika shughuli mnazofanya kwani kuna baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa sio waaminifu,” amesema Spika Ndungai.

Mbali ya wito huo, Spika Ndugai amewataka wafanyabiashara na wazalishaji kutengeneza bidhaa zenye ubora na viwango vya hali ya juu ili bidhaa za Tanzania ziweze kushindana kwenye soko la dunia na kuweza kulipatia taifa fedha nyingi za kigeni sambamba na uchangiaji ukuaji wa uchumi.

Rais wa TCCIA, Paul Koyi wa (Pili kulia) akimtambulisha Spika wa Bunge laJamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai (kulia) kwa wajumbe wa Bodi wa Chemba hiyo kwenye hafla fupi ya chakula jioni Jijini Dodoma jana. Katikati ni Mjumbe wa Bodi ya TCCIA, Eutropia James na kushoto ni Swallah Swallah.

“Sisi kama Bunge tupo tayari kufanya kazi na TCCIA kupitia Kamati yetu ya kudumu ya Viwanda, Biashara na Mazingira. Tunapenda kuona sheria na sera mbalimbali zinasaidia kukuza na kuendeleza biashara na kukuza ucchumi hapa nchini,” amesema.

Amesema Dodoma ni mkoa wa kimkakati ambao unaweza kuwekeza kwenye kilimo, viwanda vya kusindika na biashara hivyo kuiomba TCCIA kuhamasisha wafanyabiashara kuchangamkia fursa hiyo kuwekeza sambamba na azma ya serikali ya kujenga uchumi unaotegemea viwanda ifikapo mwaka 2025.

Kwa upande wake, Rais wa TCCIA, Paul Koyi mbali ya kuishukuru Serikali na bunge kwa kufanya kazi kwa kushirikiana, amesema TCCIA imekuwa mstari wa mbele katika kutoa ushauri wa namna bora ya kukuza mitaji kwa wajasiriamali, wafanyabiashara, wenye viwanda na kilimo ili kuchochea ukuaji wa uchumi na ongezeko la ajira.

“Nalishukuru sana Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa kuonyesha imani kubwa kwetu (TCCIA) kama Chema tutaendelea kufanya kazi karibu na Kamati ya Bunge kwa manufaa na maslahi mapana ya taifa,” amesema Koyi.

Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndungai (watatu kushoto) akizungumza kwenye hafla ya chakula cha jioni Jijini Dodoma juzi. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa TCCIA, Nebart Mwapwele, Wapili kushoto ni Rais wa TCCIA, Paul Koyi, Kulia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda Biashara na Mazingira, David Kihenzile, watatu kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka na wa pili kulia ni Katibu Tawala wa Mkoa huo, Dkt. Fatuma Mganga. Picha zote na mpiga picha wetu.

Amesema TCCIA iliamua kufungua ofisi Jijini Dodoma ili kupunguza gharama wanazozitumia wanachama wake pamoja na wadau wengine kufuata huduma hizo Dar es Salaam sambamba na kuongeza ufanisi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Antony Mtaka amesema Serikali imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji ili kuinufaisha nchi pamoja na muwekezaji hivyo kupiti Ofisi yake ya Mkoa inawakaribisha sekta binafsi kwenda kuwekeza katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii .

“Kama Serikali tunafanya kazi kwa karibu sana na sekta binafsi na tayari tulishaweka mazingira wezeshikupitia ofisi yangu ya mkoa. Tutatoa ushirikiano wakati wote tutakapo hitajika kwani Dodoma ni Jiji linalokua kwa kasi sana,” alisma RC Mtaka.

TCCIA ni taasisi ambayo imejipanga kumuinua mjasiriamali, mfanyabiashara wenyeviwanda na wakulima kwa kutoa ushauri wa kitaalamu wa namna bora ya kupata na kukuza mitaji yao sambamba kuchangia katika pato la taifa kwa kuzalisha ajira nyingi kwa watanzania.