April 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wazazi watakiwa kuwekeza kwenye sekta ya Elimu

Na Heri Shaaban, TimesMajira Online

DIWANI wa Viti Maalum Wanawake Wilaya ya Ilala, Mwalimu Beatrice Edward amewataka wazazi na walezi kuwekeza katika sekta ya elimu ili kuwajengea msingi bora watoto kwa ajili ya maisha ya baadaye.

Diwani Beatrice amesema hayo katika mahafali ya darasa la saba shule ya msingi Bright African yaliyofanyika katika Kata ya Mzinga.

Amesema, ili Taifa lolote liweze kupata maendeleo, wananchi wake ni lazima wasome na kupata elimu iliyo bora na sio bora elimu na kuwataka wazazi wa Wilaya ya Ilala kuunga mkono juhudi za Serikali za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuhusu Sera ya elimu bila malipo kwa kuwasomesha watoto na kufatilia maendeleo yao kitaaluma.

Amesema kuwa, wanafunzi hao ndio madaktari, wabunge na mawaziri wa baadaye hivyo ni lazima watoto walindwe na kuwasomesha ili waweze kuwa na nidhamu.

“Nawaomba wazazi na walezi kufatilia maendeleo ya watoto wetu katika sekta ya Elimu na kuwalea watoto katika misingi mema ili wawe na maadili waweze kufanya vizuri darasani na katika mitihani yao ya mkoa na ngazi ya Taifa” amesema Mwalimu Beatrice .

Pia amewataka wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kuchangamkia fursa za Serikali kwa kukopa mikopo inayotolewa na Serikali kwa ngazi ya Halmashauri ili wafanye biashara na kupata fedha za kulipa ada kwa ajili ya elimu .

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mitaa Kivule, Amos Hangaya ameishauri Serikali kupunguza kodi za ada kwa Wamiliki wa Shule Binafsi ili waweze kuziendesha shule hizo na kuisaidia Serikali katika sekta ya elimu Tanzania ikuwe akiishauri kuanza na Wilaya ya Ilala na kisha kwenye shule za Mikoani.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Bright African, Erneus Mgaya amesema, shule ya Bright African ilianza 2012 ilisajiliwa mwaka 2016 mwaka huu ni mahafali ya nne kwa darasa la saba ambapo 2018 ilishika nafasi ya nne kiwilaya, nafasi ya sita ngazi ya Mkoa, 192 ngazi ya Taifa huku 2019 nafasi ya sita Wilaya nafasi ya 40 ngazi ya Taifa.