April 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wawekezaji kutoka China kufanya uwekezaji wa Dola mil 312 nchini

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

MAZINGIRA ya uwekezaji yamewavutia wawekezaji kutoka China ambapo wameeleza kuwa wako tayari kufanya uwekezaji wenye thamani ya dola za Marekani milioni 312 (zaidi ya sh. bilioni 800) katika maeneo ya nishati, afya, ujenzi, kilimo na vifaa vya uchakataji.

Wawekezaji hao wamekutana na wadau mbalimbali kuangalia fursa za uwekezaji ikiwemo Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) ambao umewakaribisha kushirikiana katika uwekezaji.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Lumumba jijini Das res Salaam, jana, baada ya kukutana na wawekezaji hao, Katibu Mkuu wa UWT, Jokate Mwegelo, alisema wawekezaji hao ambao ujio wao umeratibiwa na Kampuni Canopus Energy Solution, wameonesha utayari wa kushirikiana katika eneo la uzalishaji wa nishati mbadala na maeneo mengine ya kimkakati.

“Chama Cha Mapinduzi kinachoongozwa na Mwenyekiti  Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kilizielekeza jumuiya zote Chama kutazama na kujiendeleza kupitia fursa mbalimbali, hii kwetu ni fursa tumejipanga kuzalisha nishati mbadala kupitia makaa yam awe.

“Wenzetu hawa wameonesha utayari, tumefanya mazungumzo ya awali na wametualika kwenda China katika maeneo yao ya uzalishaji wa huduma na bidhaa mbalimbali kujionea namna walivyo tayari kutokana na maendeleo ya teknolojia,” alisema.

Alieleza kuwa UWT ina dhamana kubwa ya kuwaendeleza wanawake wa Tanzania kupitia fursa mbalimbali, hivyo imejipanga kuunga mkono juhudi za kumtua mama kuni kichwani kwa kutengeneza mkaa mbadala ambao ni salama kwa afya za binadamu.

Kwa mujibu wa Jokate mbali na nishati mbadala, pia wanatazama uwezekano wa wa kushirikiana na wadau hao katika sekta ya madini lakini hilo litafanyika baada ya hatua mbalimbali kutekelezwa ili kuwa na ushirikiano wenye tija.

Jokate alisisitiza kwamba UWT imejipanga kutengeneza fursa ambazo zitawanufaisha wanawake katika sekta mbalimbali hususan uchumi ambao utawainua na kimaisha.

“Fursa yoyote tunayoitengeneza lengo letu ni kuona wanufaika wa kwanza wanakuwa wanawake wa Tanzania,” alisema.

Kwa upande wake Mhandisi Anna Nyangasi kutoka Kampuni ya Canopus Energy Solution, alisema ujio wa ujumbe huo ni fursa kwa uwekezaji katika sekta mbalimbali.

Anna alieleza kuwa wawekezaji hao waliongozwa na Shen Don kutoka Jimbo la Shangzhou ambapo ukiwa nchini ulikutana na wadau mbalimbali kabla ya jana kukamilisha ziara yao kwa kukutana na UWT ambapo wanaamini kuna kundi kubwa la wanawake ambalo linahitaji kuwa sehemu ya mabadiliko kutokana na uwekezaji unaoweza kufanywa na wawekezaji hao.

Kwa mujibu wa Anna, wawekezaji hao wameridhia kufanya uwekezaji wa zaidi ya dola za Marekani milioni 312 (zaidi ya sh. bilioni 800) katika maeneo ya nishati, afya, ujenzi, kilimo na vifaa vya uchakataji.

Pia, alisema ujumbe huo umeonesha nia kushirikiana na kutafuta wawekezaji katika maeneo takribani manane ambayo ni viwanda vya kuunganisha zana za kilimo (pawatila), kuzalisha vifaa vya trekta, majenereta, pampu za maji, vifaa tiba, viwanda vya bidhaa za umeme na ‘paneli’ za kuhifadhi baridi.

Mhandisi Anna alisema ujumbe huo wa watu 11 unahusisha wafanyabiashara, wawakilishi kutoka serikalini pamoja na ujumbe wa CCP, uliwasili nchini kwa mwaliko wa Canopus Energy Solution kwa kushirikiana na Kampuni ya Amec Group.

“Baada ya kuwasili kwa ujumbe huu na kufanyika mazungumzo yenye kulenga fursa za uwekezaji umekubali kuwekeza katika maeneo kadhaa ambayo ni sehemu ya mkakati wa Serikali.