April 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online DSM

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya inaendelea kuimarisha ubora wa huduma za Afya ya mama na mtoto katika vituo 25 vinavyotoa huduma ya upasuaji wa dharura wa kumtoa mtoto tumboni (CEmONC) katika Mkoa wa Dar Es Salaam ili kupunguza vifo vitokanavyo na Uzazi.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema hayo leo Machi 28, 2024 wakati akifungua mafunzo elekezi kazini juu ya huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto katika Mkoa wa Dar Es Salaam ambapo mafunzo hayo ni endelevu yanayotolewa nchini nzima ili kupunguza vifo vya mama mjamzito na mtoto.

“kuimarisha ubora wa huduma za Afya ya mama na mtoto katika vituo 25 vya Afya vinavyotoa huduma ya upasuaji wa dharura wa kumtoa mtoto tumboni yaani (CEmONC) tutakua tumetatua asialimia 84 ya changamoto za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto kwa Mkoa wa Dar Es Salaam.” Amesema Waziri Ummy

Amesema, mafunzo haya ni muhimu sana ambayo yamesaidia kupunguza vifo katika katika Mkoa wa Tabora ambapo kwa mwaka 2023 vifo vya watoto wachanga vimepungua kutoka vifo 50 hadi vifo Vinne kwa miezi Mitatu, lakini pia mafunzo hayo yanasaidia kupeana mbinu mbalimbali za kuwahudumia vizuri wagonjwa ili kuendelea kupunguza vifo vitokanavyo na Uzazi.

Aidha, Waziri Ummy amezitaka Halmashauri kutenga fedha kwa ajili ya kuwawezesha watoa huduma waliopatiwa mafunzo hayo ili waweze kwenda kutoa mafunzo hayo kwenye vituo vyao vya Afya vinavyotoa huduma ya upasuaji wa dharura wa kumtoa mtoto tumboni (CEmONC) vilivyobakia pamoja na Zahanati.

Pia, Waziri Ummy amezitaka kila Hospitali pamoja na Vituo vya Afya vinavyotoa huduma ya upasuaji wa dharura wa kumtoa mtoto tumboni (CEmONC) zianzishe wodi maalumu ya watoto wachanga inayofanya kazi kwa kuwa na vifaa tiba pamoja na watoa huduma waliojengewa uwezo.

Mwisho, Waziri Ummy amesema, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka hadi kufika Mwaka 2027 tuwe tumepunguza vifo vya watoto wachanga kutoka 24 katika kila vizazi hai 1,000 hadi kufikia 12 katika kila vizazi hai 1,000 “hii inawezekana kupitia mafunzo haya, hatutamuangusha Rais Dkt. Samia.”