May 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwandisi mchenjuaji Mandini kutoka STAMICO Happy Mbenyange (mwenye fulana ya Kijani) Akizungumza na wananchi waliofika kwenye Banda la Taasisi hiyo kujionea shughuli mbalimbali wanazofanya katika Sekta ya Madini.

Wavutiwa na teknolojia ya kutengeneza mkaa banda la STAMICO

Na David John,TimesMajira Online, Dar

OFISA uhusiano kutoka Shirika la Madini la Taifa STAMICO Bibiana Ndunguru amesema kuwa makaa ya mawe yanayotumika kutengeneza mkaa mbadala umekuwa kivutio kikubwa cha wananchi wengi wanaofika katika Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa kufika kwenye banda la Shirika la Madini la Taifa(STAMICO).

Mwandisi mchenjuaji Mandini kutoka STAMICO Happy Mbenyange akielimisha wananchi waliofika na kutembelea banda la STAMICO

Akizungumza na TimesMajira Online kwenye banda la STAMICO lililopo ndani ya jengo la Wizara ya Madini Bibiana amesema tangu yalipoanza maonesho hayo biashara kumekuwa na idadi kubwa ya wananchi wanaofika kwenye banda lao na wengi wanavutiwa na yale ambayo wamekuwa wakiyaona na kuyasikia kutoka kwa watalaamu.

“Wananchi wanakuja kuangalia sampuli za makaa ya mawe ambazo tumekuja nazo hasa makaa ambayo yanatumika kutengeneza mkaa mbadala ambayo ndio teknolojia mpya.Wanataka kufahamu kuhusu huu mkaa unafanyaje kazi, unatengenezwa na nini, na faida yake kwa ujumla na upatikanaji wake.Pia wapo wanaouliza kuhusu kiwanda cha kusafisha dhahabu kilichozinduliwa hivi karibuni.” amesema

Nakuongeza kuwa wanapokuja hapa wanataka kujua kinafanyaje kazi, dhahabu zinapatikana wapi na mwisho wa siku zinakwenda wapi na faida ya kiwanda hicho kwa Watanzania , kwa hiyo watalaam wetu wanatumia nafasi hii ya maonesho ya biashara kuwaelezea na kukusanya maoni,”amesisitiza.

Akizungumzia mkaa mbadala amesema STAMICO wamekuwa wakieleza wananchi faida zake, kwanza kabisa ni kupunguza matumizi ya mkaa unaotokana na miti ili kuzuia uharibifu wa mazingira kwani watu wengi wanatumia mkaa unaotokana na miti,hivyo miti mingi inakatwa kwa hiyo wao wanaeleza ni kwa namna gani mkaa mbadala utasaidia kutunza mazingira.

Bibiana amesema STAMICO wamekuwa wakichimba makaa ya mawe kwa hiyo yapo ambayo wanayauza makaa yakiwa mazima kulingana na mahitaji ya mteja lakini kuna vumbi linalobakia ambako hilo badala ya kuliacha kuwa uchafu wameamua kulibadilisha na kulitumia kutengeneza mkaa mbadala.

Mwandisi mchenjuaji Mandini kutoka STAMICO Happy Mbenyange

Amesema wananchi ambao wanafika kwenye banda lao wamekuwa wakiwaelimisha wananchi namna STAMICO linavyofanyakazi mbalimbali ikiwemo ya kuwekeza kwenye sekta ya madini kwa kuchimba na kuendeleza migodi inayomilikiwa na Serikali.Mpaka sasa kuna migodi miwili inayomilikiwa na Serikali ambao ni mgodi wa dhahabu wa STAMICO na mgodi wa makaa ya mawe.

Pia kuwalea na kuwaendeleza wachimbaji wadogo kwa kuwapa elimu ni kwa namna gani wanaweza kuachana na uchimbaji hatarishi na sio rafiki kwao kwa afya zao na maisha yao, pia sio rafiki kwa mazingira.”Kwa hiyo tunawataka kuachana na uchimbaji huo ili wahamie kwenye uchimbaji bora na wenye tija”.

“Kwa upande mwingine tunatoa ushauri wa kimazingira, na utafiti,tunafanya kazi za ubia katika baadhi ya migodi na shughuli zetu , kwa mfano tunaubia katika kiwanda cha dhahabu.Kuhusu mikakati yetu ni kuifanya STAMICO iwe njia au lango kuu la kuwezesha uchumi ambao unaotegemea sekta ya madini,”amesema Bibiana

Ameongeza pia kuangalia kwa namna gani wachimbaji wadogo wanaweza kunufaika kupitia STAMICO kwa kuwapa elimu ya kutosha ili mwisho wa siku waachane na uchimbaji wenye athari, waje kwenye uchimbaji mzuri.

“STAMICO tunataka kuleta uchimbaji mdogo wenye tija , pia tunataka kuifanya sekta ya madini kuwa na manufaa kwa jamii ili isiwe tu sekta ya madini inawanufaisha watu wachache, ndio maana unaona tunajitahidi kutafuta wawekezaji kuja kuwekeza kwenye sekta ya madini, tumejenga kiwanda cha kusafisha madini na teknolojia ambayo inatumika pale itabaki pia kwa Watanzania.

Amesema kwenye banda lao kuna kundi la wachimbaji wenye usikivu hafifu ambao waliwakusanya pamoja kutoka kanda ya ya ziwa kutoka Wilaya ya Sengerema, Geita, Mwanza , Chato na maeneo mengine ya kanda ya ziwa.Tuliwachukua na kuwapa elimu ya uchimbaji mdogo ambao ni salama, hivyo walikuwepo hapa, wanaelezea kwa namna gani wananuifaka na uwepo wa STAMICO.

Kauli ya STAMICO kwa Watanzania wanaokwenda kwenye banda lao, wamewaomba wawe mabalozi wazuri kwa wengine baada ya kupata kila aina ya ufafanuzi kutoka kwa watalaamu wao.

“Pia tunatumia nafasi hii kukusanya maoni, hivyo tutaendelea kuyapokea lengo letu ni kuijenga STAMICO yetu kwa manufaa ya Watanzania wote,” amesema.