Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online-Dar
MKUU wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo, amewataka Watendaji wa Halmashauri ya Jiji la Dar-es-Salaam kufanya kazi kwa weledi na kusimamia miradi ya Serikali iweze kukamilika kwa wakati huku akiwaonya juu ya vitendo vya rushwa.
Mpogolo ametoa agizo hilo wakati alipokuwa katika Kata za Chanika na Zingiziwa wilayani Ilala kwenye kampeni ya kupanda miti na usafi wa mazingira.
Ambapo amesema,kazi ndio kipimo kikubwa cha uongozi hivyo wanapaswa kukaa na kujadili namna ya kufanya kazi vizuri na kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na wananchi wanapata huduma bora.

Amesisitiza kuwa si vizuri viongozi au watendaji kukaa na kujadili ni asilimia ngapi ya fedha wanapata kutokakana na mikataba au miradi ya Serikali.
Mpogolo amesema,kila kiongozi au mtendaji ana wajibu wa kuhakikisha fedha zinazotengwa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa barabara au miundombinu ya sekta ya afya,elimu na huduma zingine zinatumika kwa uadilifu ,uwazi na kwa kuzingatia thamani ya fedha (value for maney)ili wananchi waweze kupata manufaa yaliokusudiwa.
Amesema Halmashauri ya Jiji la Dar-es-Salaam na Wilaya ya Ilala imeona nidhamu na uadilifu katika usimamizi wa fedha,hivyo alitumia fursa hiyo kuwapongeza viongozi wa halmashauri hiyo huku akiwataka wasibweteke waendelee kuchapa kazi na kuwa wadilifu kwa sababu uadilifu ndio msingi wa Serikali yenye kuwajibika.
Alitumia fursa hiyo kuwataka viongozi kujenga utamaduni wa kufanya kazi kwa kushirikiana,kusimamia miradi ya maendeleo ya Serikali na kuhakikisha kila rasilimali inayotolewa inalenga kuboresha maisha ya wananchi na si kutengeza maslahi binafsi.
Hata hivyo aliwataka watendaji wa Serikali kuanzia ngazi ya Serikali ya mtaa hadi wilaya kuwa karibu na wananchi na kusikiliza pamoja na kushughulikia changamoto zao kwa wakati kwani wameaminiwa ili wawe sehemu ya suluhisho la kutatua kero zao.


More Stories
Tabora kulipa mil.27 za HESBL
DC Chato: Osha ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi
Viongozi wa Dini watakiwa kuhubiri maadili mema