Na Mwandishi Wetu,TimesMajira
MKUU wa Wilaya ya Chato, Louis Peter Bura, amesema kasi kubwa ya ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika Mkoa wa Geita imeongeza uhitaji wa huduma za usalama na afya mahali pa kazi, akiiomba Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kuongeza huduma za ukaguzi, mafunzo na ushauri wa kitaalamu katika maeneo ya kazi.
Bura ametoa kauli hiyo wakati akifungua mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi yaliyotolewa na OSHA kwa kikundi cha mafundi wanaojihusisha na uchomeleaji wa vyuma na useremala katika Kijiji cha Kalebezo, Kata ya Nyamirembe, Wilaya ya Chato, Mkoa wa Geita.
Mafunzo hayo, yaliyofanyika mwishoni mwa wiki ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa OSHA na yalihudhuriwa na watu 15 kutoka kikundi cha Smart Welders and Furniture, ambacho kituo chake hutumika pia kutoa mafunzo ya ufundi kwa wananchi wa Kata ya Nyamirembe na maeneo ya jirani.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Bura amesema katika kipindi cha miaka mitatu tangu mwaka 2024, Wilaya ya Chato imeshuhudia ongezeko kubwa la shughuli za kiuchumi, ikiwemo shughuli za uchimbaji wa madini, hali inayoongeza umuhimu wa kuhakikisha mazingira ya kazi yanakuwa salama na yenye afya.
“Kipekee niwashukuru sana OSHA kwa kuendelea kutekeleza ipasavyo jukumu lenu la msingi la kusimamia usalama na afya katika maeneo ya kazi nchini. Lakini naomba niwakumbushe kwamba maeneo mengi yanayokuwa kiuchumi yanahitaji sana huduma zenu. Mkoa wa Geita, hususan Wilaya ya Chato, ni miongoni mwa maeneo hayo,” amesema Bura.
Amesema OSHA inapaswa kuyapa kipaumbele maeneo yenye kasi kubwa ya ukuaji wa shughuli za kiuchumi, akieleza kuwa wananchi na waajiri kwa sasa wanaendelea kutambua umuhimu wa huduma zinazotolewa na taasisi hiyo.

“Hivyo, niwaombe kuyaangalia maeneo haya kwa jicho la pekee. Huko nyuma huenda OSHA haikujulikana kwa watu wengi, lakini kwa sasa watu wanatambua umuhimu wenu na wanahitaji huduma zenu za ukaguzi wa mifumo ya usalama na afya, uchunguzi wa afya za wafanyakazi, mafunzo pamoja na ushauri wa kitaalamu kuhusu uboreshaji wa mazingira ya kazi,” amesema.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya ameipongeza OSHA kwa kutoa mafunzo pamoja na msaada wa vifaa kinga kwa kikundi hicho cha mafundi, akisema shughuli wanazofanya zinahusisha matumizi ya mashine na vifaa vinavyoweza kusababisha madhara endapo hatua stahiki za usalama hazitazingatiwa.
Bura ameahidi kuwa Serikali ya Wilaya itaendelea kushirikiana na OSHA katika kuhamasisha wakazi wa Chato kuzingatia kanuni na taratibu bora za usalama na afya katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Pia amewataka wamiliki na waendeshaji wa maeneo ya kazi kutoa ushirikiano kwa wataalamu wa OSHA ili kuwezesha ukaguzi, utoaji wa elimu na ushauri wa kitaalamu kwa lengo la kuimarisha usalama na afya mahali pa kazi.
Kwa upande wake, Meneja wa OSHA Kanda ya Ziwa, Lodgard Bishanga, amesema mafunzo hayo yalilenga kuwajengea washiriki uelewa kuhusu vihatarishi vya kiusalama na kiafya vinavyoweza kujitokeza katika shughuli zao za uchomeleaji na useremala, pamoja na kuwafundisha namna ya kuvitambua na kuchukua hatua za kuvidhibiti.
Bishanga amesema utoaji wa elimu hiyo ni sehemu ya juhudi za OSHA za kuhakikisha wafanyakazi na waajiri wanakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu umuhimu wa kuzuia ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.
“Sambamba na kupatiwa mafunzo, washiriki wamekabidhiwa vifaa kinga vya mfano, vikiwemo makoti ya usalama, glovu, kofia ngumu na barakoa. Vifaa hivyo vimegharamiwa na Serikali kama sehemu ya kuendelea kuhamasisha uzingatiaji wa kanuni bora za usalama na afya katika shughuli za uzalishaji,” amesema Bishanga.
Amesema matumizi sahihi ya vifaa kinga ni hatua muhimu katika kupunguza uwezekano wa wafanyakazi kupata majeraha au madhara ya kiafya yanayoweza kusababishwa na mazingira ya kazi.
WASHIRIKI WASEMA MAFUNZO YAMEWASAIDIA
Kwa upande wao, washiriki wa mafunzo hayo, akiwemo Lulinda Makoye Manyema na Neema Kalebo, wameishukuru Serikali kupitia OSHA kwa kuwapatia elimu kuhusu usalama na afya mahali pa kazi pamoja na vifaa kinga.
Neema Kalebo amesema mafunzo hayo yamewasaidia kupata uelewa zaidi kuhusu namna ya kuboresha usalama katika karakana zao na kuchukua hatua za haraka endapo ajali itatokea.
“Tumejifunza mambo mengi sana kupitia mafunzo haya, ikiwemo jinsi ya kukuza na kulinda usalama tunapokuwa katika karakana zetu, pamoja na kuwa na mpangilio mzuri wa mashine na vifaa. Aidha, tumejifunza jinsi ya kutoa huduma ya kwanza endapo itatokea ajali katika shughuli zetu za kila siku,” amesema Kalebo.

More Stories
Tabora kulipa mil.27 za HESBL
Watendaji watakiwa kufanya kazi kwa weledi
Viongozi wa Dini watakiwa kuhubiri maadili mema