April 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

amanda wa Polisi Mkoani Mbeya Ulrich Matei

Wanne mbaroni kwa tuhuma za kumuua muuguzi

Na Esther Macha, Timesmajira,Online, Mbeya

JESHI la Polisi mkoani Mbeya linawashikilia watu wanne kwa tuhuma za kumuua kwa kumchoma na kisu maeneo mbal mbali ya mwili wake Muuguzi wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya ,Annah Jakobo (51) .

Kamanda wa Polisi Mkoani Mbeya Ulrich Matei

Kamanda wa Polisi Mkoani Mbeya ,Ulrich Matei amesema kuwa tukio hilo limetokea Agosti 25, mwaka huu, majira ya saa 16.00 jioni katika mtaa wa Manga-Veta,Kata ya Ilomba Jijini Mbeya ambapo Muuguzi huyo alikutwa nyumbani kwake anakoishi peke yake akiwa ameuwawa kwa kuchomwa kisu tumboni ,kifuani,sikioni,pajani, na kwenye kitovu .

Hata hivyo Matei amesema kufuatia tukio hilo Polisi inawashikilia watu wanne ambao ni Kolosani Samson (25)ambaye ni fundi ujenzi na mkazi wa Mbalizi ,Hussein Dickson (25),Isaya Mwalusanya(30) pamoja na Said Hassan (34) ambao wote ni wakazi wa Mbalizi Jiji ni Mbeya.

Akielezea zaidi Kamanda Matei amesema marehemu alitoka kazini Agosti 24, mwaka huu,majira ya saa 06:30 asubuhi na alitakiwa kuingia tena kazini saa 18:30 jioni lakini hakuonekana kazini hadi 25/8/2020 majira ya saa 16:30 jioni alipokutwa ameuawa ndani ya nyumba yake huko Manga Veta.

Aidha Matei alisema kwamba kufuatia tukio hilo, kikosi kazi cha kuzuia na kupambana na uhalifu Wilaya ya Mbeya Mjini kilianza msako mara moja wa kumtafuta mtuhumiwa na mnamo Agosti 30,mwaka huu, majira ya saa 22:00 usiku huko Kijiji na Kata ya Iyula, Wilaya ya Mbozi, Mkoa wa Songwe alikamatwa Kolosani Samson (25)na baadae walikamatwa wenzake watatu kuhusiana na tukio hilo.

Kamanda Matei alisema chanzo cha tukio hilo ni kwamba mtuhumiwa alikuwa anadai fedha sh. 500,000 baada ya kufanya kazi ya kuremba madirisha 12 kwa makubaliano ya sh.50,000 kwa kila dirisha katika nyumba ya marehemu na awali alilipwa kiasi cha sh.100,000.

Siku aliyofuatilia deni lake nyumbani kwa marehemu alimkuta akiwa anaosha vyombo na alipomueleza madai yake ulizuka mzozo kati yao ndipo mtuhumiwa alimuua kwa kumchoma kisu sehemu mbalimbali za mwili.

Aidha watuhumiwa wengine watatu waliokamatwa walikutwa na simu moja Smartphone aina ya Samsung mali ya marehemu na kuwa upelelezi wa shauri hilo unaendelea na mara baada ya kukamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani.