May 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi waghairi kuihama halmashauri baada ya kupata maji

Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Korogwe

WANANCHI wa Kijiji cha Kwemasimba, Kata ya Vugiri, Tarafa ya Bungu wamesitisha zoezi la kuomba kuhamishwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe kwenda Halmashauri ya Mji Korogwe mkoani Tanga, baada ya kuanza kupata maji.Kwa zaidi ya miaka 10, wananchi hao walikuwa wanataka kuhamishwa kiutawala kwenda Kata ya Mtonga, Halmashauri ya Mji Korogwe ili kupata huduma za kijamii ikiwemo maji, umeme, barabara na zahanati, kwani huko waliko sasa wamekosa huduma hizo.

Walitoa hakikisho hilo la kubaki Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Desemba 19, 2022 mbele ya Meneja wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (RUWASA) Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo alipofika kijijini hapo kukagua mradi wa maji, ambao baadhi ya vituo vya maji (vilula) vimeanza kutoa maji.

“Sasa tumeondoa tishio la kutaka kuondoka Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe kwenda Halmashauri ya Mji Korogwe sababu Serikali imeanza kutuletea huduma za jamii baada ya kuanza kupata maji ya bomba. Sasa kilichobaki ni umeme na barabara.”

“Tunatska Serikali ituletee umeme na barabara ya uhakika. Wananchi wanapata shida sana na usafiri wa kwenda mjini Korogwe na maeneo mengine ya nchi, lakini kama tutatengenezewa barabara ya uhakika itatusaidia sana” alisema Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mbalamo Suleiman Mshihiri.

Naye Mjumbe wa Kamati ya Mazingira Kijiji cha Kwemasimba Godfrey Kidudu alisema kwa sasa wanachotaka kwenye kijiji chao ni huduma za jamii tu.

Tayari wana maji ya bomba, lakini wanataka umeme na kutengenezewa barabara. Pia kutaka msaada wa kujengewa zahanati, kwani tayari wana eneo lao wameanza kuchimba msingi kwa ajili ya zahanati hiyo.

Akizungumza na wananchi wa kijiji hicho wakiwemo Wajumbe wa Serikali ya Kijiji, Mhandisi Lugongo aliwataka wananchi kutunza vyanzo vya maji, kwani miradi hiyo ya maji inayojengwa itakuwa haina faida kama vyanzo vya maji vitakuwa vimekauka, hivyo viongozi wa vijiji washirikiane na wananchi kuweza kutunza vyanzo hivyo.

“Nimefurahi hapa kuona kuna viongozi wa mazingira. Tunaomba viongozi wa mazingira kuwahamasisha wanafunzi kuanza kupenda kutunza mazingira kwa kupanda miti. Mtu ana watoto watano, kila mtoto unampa mti wa kupanda kuzunguka nyumbani kwao, hiyo itasaidia kurudisha uoto wa asili” alisema Mhandisi Lugongo.

Mhandisi Lugongo pia aliwaasa wananchi hao kuwa baada ya mradi wote kukamilika, wataanza kuchangia kwa kulipia maji kiasi cha fedha ili miradi ya maji iwe endelevu, sababu kukitokea matengenezo ya bomba ama koki, basi vifaa hivyo viweze kununuliwa kwa fedha za mfuko wa maji wa kijiji.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mara baada ya ziara hiyo, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Korogwe Mhandisi William Tupa, alisema Mradi wa Maji Kwemasimba hadi kukamilika kwake utagharimu sh. milioni 481, na maji hayo yatafika kwenye vitongoji vyote vitano vya kijiji hicho ambavyo ni Uzimba, Kwemasimba, Nkwamba, Mbalamo na Antakaye.

“Mradi huo hadi kukamilika kwake, utagharimu sh. milioni 481, huku ukiwa na tenki la lita 75,000 na vituo vya kuchota maji (vilula) 10, na kwa sasa wananchi 2,731 watanufaika na mradi huo, lakini uwezo wa mradi huo ni kuhudumia wananchi 4,313, hivyo kuwa na uwezo wa kuhudumia wananchi hadi mwaka 2041” alisema Mhandisi Tupa.

Mhandisi Tupa alisema mradi mwingine, ambao uliweza kutembelewa na Meneja wa RUWASA Mhandisi Lugongo ambao pia aliridhika na maendeleo yake ni Mradi wa Maji Makuyuni.

Mradi huo utahudumia vijiji vitatu ambavyo ni Makuyuni, Gomba/Lamu na Madumu, na utagharimu sh. bilioni 1.4 hadi utakapokamilika.

Mhandisi Tupa alisema mradi huo utakaohudumia wananchi 9,460, utakuwa na vituo vya kuchotea maji (vilula) 30, na tenki linalojengwa ambalo lipo hatua za mwisho kukamilika, litakuwa na ujazo wa lita 300,000.

Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo (kulia) akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kwemasimba, Wilaya ya Korogwe alipofika kwenye moja ya vituo vya maji (kilula) ikiwa ni ziara ya kutembelea miradi ya maji wilayani humo. Wa pili kulia ni Meneja wa RUWASA Wilaya ya Korogwe Mhandisi William Tupa. (Picha na Yusuph Mussa).

Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo (kulia) akisaidiwa na mmoja wa Wahandisi wa RUWASA Wilaya ya Korogwe France Malya ili kupanda mlima ili kufika na kukagua tenki la maji linalojengwa Kijiji cha Kwemasimba, Wilaya ya Korogwe alipofika kijijini hapo kwenyei ziara ya kutembelea miradi ya maji wilayani humo. (Picha na Yusuph Mussa).

Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo akijiridhisha kuwa tenki la kuhifadhi maji Kijiji cha Kwemasimba, Wilaya ya Korogwe lina maji. Ni baada ya kufika kijijini hapo kwenyei ziara ya kutembelea miradi ya maji wilayani humo. (Picha na Yusuph Mussa).
Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo (katikati) alipofika Kijiji cha Makuyuni, Kata ya Makuyuni, Wilaya ya Korogwe Desemba 19, 2022 kukagua Pump House kwa ajili ya Mradi wa Maji Makuyuni ambao utanufaisha wananchi zaidi ya 9,000 wa vijiji vitatu vya Gomba/Lamu, Makuyuni na Madumu. Wa pili kulia ni Meneja wa RUWASA Wilaya ya Korogwe Mhandisi William Tupa. (Picha na Yusuph Mussa).
Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo (katikati) akipata maelezo kutoka kwa Meneja wa RUWASA Wilaya ya Korogwe Mhandisi William Tupa (kushoto) alipofika Kijiji cha Makuyuni, Kata ya Makuyuni, Wilaya ya Korogwe Desemba 19, 2022 kukagua tenki lenye ujazo wa lita 300,000 kwa ajili ya Mradi wa Maji Makuyuni ambao utanufaisha wananchi zaidi ya 9,000 wa vijiji vitatu vya Gomba/Lamu, Makuyuni na Madumu. (Picha na Yusuph Mussa).
Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo (kushoto) akipata maelezo kutoka kwa Meneja wa RUWASA Wilaya ya Korogwe Mhandisi William Tupa (katikati) alipofika Kijiji cha Makuyuni, Kata ya Makuyuni, Wilaya ya Korogwe Desemba 19, 2022 kukagua jengo la Watumiaji Maji kwa ajili ya Mradi wa Maji Makuyuni ambao utanufaisha wananchi zaidi ya 9,000 wa vijiji vitatu vya Gomba/Lamu, Makuyuni na Madumu. (Picha na Yusuph Mussa).