April 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NAIBU Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mussa Sima

Waliojenga msitu wa Slender kuchukuliwe hatua

Na Mwandishi Wetu

NAIBU Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mussa Sima amechukizwa na ujenzi wa nyumba katika eneo la Msitu wa Asili wa Slender alilolitembelea jana Jijini Dar es Salaam na ameagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira nchini (NEMC) liwachukulie hatua watu ambao wamejenga na kufanya shughuli nyingine za kibinadamu katika eneo hilo.

Waziri ametembelea eneo la mikoko kando ya daraja la Slender baada ya kuwepo taarifa za kuendelea kwa shughuli za kibinadamu katika msitu huo wa asili ikiwemo ujenzi wa nyumba na utiririshaji wa maji taka baharini, wakati Serikali inajenga daraja refu la kisasa ili kulifanya Jiji la Dar es Salaam liwe na mvuto wa kimataifa.

“Eneo la Slender ni miongoni mwa maeneo ya kimkakati katika utunzaji wa mazingira kama yalivyo maeneo mengine kote nchini yenye uoto wa asili. Eneo hili lipo ndani ya hifadhi ya mazingira na Serikali haitakubali kuona shughuli zozote za kibinadamu zikiendelea katika eneo hili pamoja na maeneo mengine muhimu kote nchini,’’ amesisitiza Waziri Sima.

Sima ameitaka NEMC kufuatilia kwa karibu watu wote ambao wamefanya shughuli za kibinadamu katika eneo hilo na kuwachukulia hatua za kisheria.

“Kumekuwepo na shughuli za kibinadamu katika eneo hili ikiwemo ujenzi na utiririshaji wa maji taka ambayo yanaingia baharini na kuleta madhara kwa viumbe wanaoishi majini.

Naliagiza Baraza kuwatafuta watu wote ambao wamekuwa wakifanya shughuli hizo na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria,’’ amesema.

Sima ametoa wito kwa Watanzania kutunza mazingira ikiwemo maeneo maalumu ambayo yametengwa na Serikali kama sehemu ya maeneo ya uoto wa asili.

“Yanayofanyika hapa ndiyo yanayofanyika katika maeneo mengi yaliyotengwa na Serikali hapa nchini. Tumejipanga kuyalinda mazingira na yeyote atakayebainika kuyaharibu sheria itachukua mkondo wake,’’ amesema.

Mkurugenzi wa Sheria wa NEMC, Benard Kongola, ameeleza kuwa eneo hilo limekuwa na mgogoro kwa muda mrefu kidogo na kwamba baraza limekuwa likichukua hatua kuhakikisha hakuna shughuli zozote zinafanyika katika eneo hilo.

“Pamoja na maagizo ya Waziri ambayo tutayafanyia kazi mara moja, tunapendea ieleweke kwamba Baraza limekwishawaripoti watumishi wa Baraza ambao walishikiriana na wanufaika wa eneo hili kughushi nyaraka za kurasimisha eneo hilo kwa shughuli za kibinadamu,’’ ameeleza Bw. Kongola.

Amesema NEMC pia wamekuwa wakitembelea eneo hilo mara kwa mara kukagua mazingira ya eneo hilo na kuchukua hatua ikiwemo kuwapiga faini wanaotiririsha maji machafu baharini.

Amesema mbali ya kuwapiga faini wakazi waliobainika kutiririsha maji katika msitu huo, NEMC imewaelimisha njia nzuri za kutumia kulinda mazingira ili maji machafu yasiingie baharini na kuathiri viumbe vya baharini.

Baraza linachukua hatua za kimkakati kulinda mazingira na kuungamkono azma ya Serikali ya ujenzi wa viwanda.