May 4, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waipongeza serikali kupata huduma ya macho

Na Mwandishi wetu, Mbarali

Wakazi wa Wilaya Mbarali mkoani Mbeya wameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Afya na wadau wa huduma za macho kwa kuwapatia matibabu ya macho bila malipo.

Akizungumza katika kambi ya upasuaji wa mtoto wa jicho inayoendelea kwenye hospitali ya Wilaya Mbarali Antony Ndwenywa(83) kutoka kitongoji cha Mkanyageni-Rujewa ambaye alifanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho kwa macho yake mawili Disemba 2022.

Ambapo amesema tangu amefanyiwa upasuaji anaendelea vizuri na hivi sasa anasoma hata magazeti.

“Mimi nilifanyiwa upasuaji wa macho yote mawili yalikuwa na mtoto wa jicho na hadi sasa naendelea vizuri…..,tunaishukuru Serikali kwa kutupatia huduma sisi watu wa chini ambazo ni bila malipo,”amesema Ndwenywa.

Vailet Mbelewele Mkazi wa Mabadaga ambaye alikua na mtoto wa jicho kwa muda wa mwaka mmoja amewashukuru watoa huduma wakiwemo madaktari na wauguzi kwa huduma nzuri walizompatia ametolewa bandeji na sasa anaona.

Amesema mara baada ya kupata tatizo hilo alikua akinunua dawa kwenye maduka bila ushauri wa madaktari. “Nawashauri wananchi wasijinunulie dawa mje moja kwa moja kwani madaktari wapo na huduma ni nzuri”.

Kwa upande wake Ahmed Abdallah Mkazi wa Igurusi ambaye alifanyiwa upasuaji wa jicho moja miaka miwili iliyopita na kwa kambi hiyo amefanyiwa upasuaji jicho la pili amemshukuru Rais Samia pamoja na viongozi wake wa chini kwa jitihada zake kwa kuwasaidia watu wa chini.

“Tunamshukuru mama kwa kutusaidia mambo mengi kama barabara,ametuletea mbolea,natoa sifa kwa Dkt. Samia anatuhudumia sisi watu wa hali hii kwani habagui na hachagui,”.

Kambi ya upasuaji wa mtoto wa jicho wilayani Mbarali imeanza Aprili,11, hadi 20,2023 na inaratibiwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Hellen Keler International la nchini hapa.