April 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wahitimu Sunshine watia fora masomo ya sayansi

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online, Kibaha

WAHITIMU wa kidato cha nne wa shule ya Sunshine ya Kibaha Mkoa wa Pwani wametia fora kwa namna walivyoweza kuelezea masomo ya baiolojia na uhandisi wa umeme kana kwamba ni wakufunzi waliokwisha kuhitimu kwenye masomo hayo.

Hayo yalitokea kwenye mahafali ya 14 ya shule hiyo yaliyofanyika shuleni hapo Mkoa wa Pwani na kuhudhuriwa na wazazi na walezi wa wanafunzi hao.

Rogers Titus na wenzake waliweza kuwashangaza wageni kwenye mahafali hayo kwa namna walivyomudu kuelezea moyo wa binadamu unavyofanyakazi na kisha kuufanyia upasuaji.

Hali hiyo iliibua shangwe kwa wageni waalikwa kutokana na namna, Rogers na wenzale walivyokuwa wakimudu kujielezea kwa ufasaha kwa kutumia lugha ya kingereza kuhusu moyo unavyofanya kazi na kisha kuupasua.

Mhitimu wa kidato cha nne wa shule ya Sunshine ya Kibaha Mkoa wa Pwani, Titus Rogers akionyesha umahiri wa kuelezea moyo wa binadamu unavyofanyakazi wakati wa mahalai ya 14 ya shule hiyo yaliyofanyika Jumamosi mkoani humo.

Wanafunzi wengine walionesha umahiri kwenye masuala ya umeme baada ya kuonesha namna wanavyoweza kutengeneza umeme kwa kutumia vifaa mbalimbali walivyobuni wenyewe.

Wakati huo huo, wanafunzi wanaosoma shule za St Anne Marie Academy ikiwemo Sunshine ya Kibaha watakaofiwa na wazazi wao na kushindwa kulipa ada ya hawatafukuzwa shule na badala yake wataendelea na masomo kama kawaida.

Ahadi hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi wa shule ya Sunshine, Jasson Rweikiza kwenye mahafali ya 14 ya shule hiyo yaliyofanyika shuleni hapo Kibaha Mkoa wa Pwani.

Amesema kwa mwaka huu pekee wazazi 93 wamefariki dunia kwasababu mbalimbali na kusababisha baadhi ya wanafunzi kuacha masomo kwa kukosa ada.

“Tumekuwa tukipoteza wazazi wengi na mwezi huu pekee tumepoteza wazazi watatu na hali hii imekuwa ikiathiri sana wanafunzi, lakini kuanzia sasa hakuna atakayefiwa ambaye atafukuzwa shule kwa kukosa ada,” alisema

Wanafunzi wa kidato cha nne wa shule ya sekondari ya Sunshine ya Kibaha Mkoa wa Pwani wakielezea namna mfumo wa umeme wa solar unavyofanya kazi wakati wa mahafali yao yaliyofanyika Jumamosi mkoani hapo.

” Kama yuko darasa la kwanza ataendelea kusoma mpaka darasa la saba na kama ni sekondari ataendelea mpaka kidato cha nne,” amesema Dkt. Rweikiza ambaye ni Mbunge wa Bukoba Vijijini CCM

Dkt. Rweikiza amesema katika mpango wa kuinua taaluma shuleni hapo wameaandaa zawadi mbalimbali zikiwemo fedha taslimu kwa awatakaofanya vizuri kwenye masomo yao.

Amesema mwanafunzi atakayepata daraja la kwanza atapata sh 600,000 na atakayepata daraja la II atapata Sh 200,000 na kwamba lengo ni kuhakikisha hakuna daraja la nne wala daraja la tatu shuleni hapo.

Mkuu wa shule ya Sunshine, Frank Raphael alisema wahitimu hao wameandaliwa vizuri kitaaluma na wanatarajiwa kufanya vizuri kwenye mitihani yao.

Amesema wanafunzi hao wamewezeshwa kufikia hapo na walimu wenye taaluma na uzoefu wa kutosha huku akimshukuru Mkurugenzi wa shule hizo, Dk. Rweikiza kwa kuendelea kufanya maboresho.

Mkurugenzi wa shule za St Anne Marie Academy zinazomiliki shule hiyo ya Sunshine ya Kibaha akilishwa keki na mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo kwenye mahafali yaliyofanyika Jumamosi shuleni hapo.

Amesema Dkt. Rweikiza aliwawezesha kupata maabara iliyosheheni vifaa vya kutosha, vifaa vya kufundishia kama vitabu, projekta, mashine ya kudurufia, maji safi, ulinzi na huduma bora za afya.