April 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TADB yaunga mkono juhudi za Serikali kupambana na Uviko-19

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online, Dar

KATIKA kuhakikisha afya ya wafanyakazi na wadau wake zinaimarika sambamba na kujenga uchumi imara wa taifa, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa kushirikiana na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imefanikiwa kuratibu na kutoa elimu ya Uviko -19 pamoja utoaji wa chanjo kwa wadau mbalimbali wakiwemo wafanyakazi wa benki hiyo Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa zoezi hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Frank Nyabundege alisema benki hiyo inaunga mkono juhudi za Serikali kupambana na uviko -19 jambo ambalo limeisukuma benki yake kushirikiana na JKCI kuratibu zoezi hilo kutoa fursa kwa wadau wake kupata elimu na chanjo sahihi ili kulinda nguvu kazi kwenye sekta ya kilimo ambayo imeajiri takribani asilimia 60 ya Watanzania wote.

“Leo tumepata wasaa mzuri wa kuweza kuendesha zoezi hili lakini lengo hasa la zoezi hili ni kuona elimu kuhusu janga hili la Uviko-19 inawafikia wadau wengi na hata huduma ya kuchanja wanaipata hapahapa tena kwa wakati ili kuokoa nguvu kazi hii kubwa kwa taifa”, alisema Bw. Nyabundege.

Aliongeza kuwa “TADB inatekeleza malengo ya Serikali ya kuanzisha chanjo tembezi ambayo itaongeza idadi ya vituo vya chanjo kutoka vituo 550 hadi kufikia vituo 6,784 jambo ambalo linatoa fursa wafanyakazi na familia zao kupata huduma hiyo kwenye makao makuu ya ofisi hizo bila gharama zozote”.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya kilimo Tanzania (TABD), Frank Nyabundege, akipata chanjo ya Uviko-19 katika uzinduzi wa mafunzo ya chanjo kwa hiari(Chanjo tembezi) yaliyofanyika Makao makuu ya ya Benki hiyo Jijini Dar es salam mwishoni mwa wiki kwa kushirikiana na Taasisi ya Moyo ya Jakaya kikwete (JKCI). Hatua hiyo inalenga kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuambana na ugonjwa wa Uviko 19 na kuhamasisha wananchi kujitokeza ili kupata chanjo na kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo. Kushoto ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Dkt. Rashid Mfaume.

Aidha Nyabundege alichukua fursa hiyo kuwahimiza wadau wa sekta ya kilimo nchini kujitokeza kwa wingi kwenye vituo vilivyoainishwa nchi nzima ili waweze kujikinga na athari za ugonjwa huo ikiwemo kupoteza maisha.

“Kwa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) inasemekana mpaka sasa watu takribani milioni 4,697,099 wamepoteza maisha kutokana na athari ya ugonjwa huu, hivyo basi kwa umuhimu mkubwa niwaombe watanzania wenzangu kushiriki kikamilifu kupata chanjo ili tuondokane na hatari ya kupoteza maisha pindi utakapo pata ugojnwa huu”, alisema Bw. Nyabundege.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Rashid Mfaume aliipongeza TADB na JKCI kwa kuratibu zoezi hilo na kuwataka wadau mbalimbali nchini kuondoa dhana potofu juu ya chanjo ya ugonjwa huo.

“Mimi niapenda kuipongeza benki na hata JKCI kwa ushirikiano huu unaowezesha watu kupata chanjo lakini napenda niwaondoe wananchi wetu hofo kuwa chanjo hii ni salama na ndio chanjo sahihi itakayowezesha mtu yeyeto atakayechoma awe salama na kuondokana na hatari ya kupoteza uhai pindi atakapo ugua ugojnwa huu,” amesema Dkt. Mfaume.

Amesisitiza kuwa; “Maendeleo yeyote yale katika taifa lolote lile yanaendana na uwepo wa nguvu kazi yenye afya bora hivyo tujitokeze kwa wingi kupata chanjo kwa faida ya familia yako na hata taifa”.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TABD), Frank Nyabundege, akisisitiza jambo kwenye uzinduzi wa mafunzo ya Uviko-19 na zoezi la chanjo kwa hiari (Chanjo tembezi) yaliyofanyika Makao Makuu ya Benki hiyo Jijini Dar es Salaam mwisho kwa kushirikiana na Taasisi ya Moyo ya Jakaya kikwete (JKCI) ikilenga kuunga mkono juhudi za Serikali katika kupambana na ugonjwa wa Uviko 19 na kuhamasisha wadau wake na wananchi kwa ujumla kujitokeza ili kupata chanjo na kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo.

Naye Mkurugenzi wa Kurugenzi wa Magonjwa ya Moyo wa JKCI, Dkt. Tatizo Waane, mbali ya kuoto elimu ya umuhimu wa chanjo kwenye zoezi hilo, amewahamasisha watu kujitokeza kuchanja kwa kuwa chanjo hiyo ni sawa tu na chanjo zingine ambazo zinatolewa kwa lengo la kuthibiti athari kubwa ya ugonjwa huo.

“Chanjo hizi hazina madhara yoyote ile ni sawa tu kama chanjo zingine na sisi kama wataalamu tunaendelea kusisitiza watu wachanje kwa wingi ili tuweze kupunguza athari za uviko- 19”, alisema Dkt. Waane.