Na Mwandishi wetu,Timesmajira Online-Mbeya
SERIKALI kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kwa kushirikiana na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), imeanza kutekeleza mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabianchi kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa maziwa, kuwawezesha wafugaji kupata elimu na mbegu bora za mifugo.
Mradi huo unalenga kukabiliana na changamoto ya upatikanaji mdogo wa malighafi kwa ajili ya usindikaji wa maziwa na kuhakikisha maziwa salama yenye ubora yanapatikana,hatua inayotarajiwa kupunguza utegemezi wa maziwa yanayoagizwa kutoka nje ya nchi.

Akizungumza Agosti 12,2026 Mkurugenzi wa Uzalishaji na Maendeleo ya Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Steven Michael, wakati wa ziara ya kutembelea vikundi vinavyotarajiwa kunufaika na mradi huo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, mkoani Mbeya.
“Ni mradi ambao unaongeza uzalishaji kwa tija kwa kuzingatia sasa hivi tuna Dira 2050,ambayo inataka sekta za uzalishaji ziweze kuhakikisha zinachangia asilimia 10,ya lengo la kufikia uchumi wa trilion moja ya dola za kimarekani,”amesema Mkurugenzi huyo.
Michael amesema,sekta za uzalishaji ikiwemo ya Mifugo na Uvuvi inatakiwa zichangie kwa kuongeza tija pamoja na kuongeza thamani ya mazao yake na mradi huo wa maziwa unatekelezwa kwa maeneo yao Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ,Kaskazini pamoja na Kanda ya Ziwa .
Amesema,mradi huo una maeneo makubwa mawili kuongeza tija kuwa na mifugo bora ,upatikanaji wa maji na malisho pamoja na kuthibiti magonjwa pia kuzalisha mazao yanayoendana na soko na kuongeza thamani ya mazao.
“Tuna viwanda vyenye uwezo mkubwa wa kusindika maziwa lakini vina changamoto ya malighafi,hivyo tunategemea kuwa mradi huu utakuwa suluhisho kwa wafugaji wetu kwa kupata mbegu bora za mifugo na kutoa mafunzo kwa wafugaji ili mwisho wa siku tuweze kuzalisha maziwa yaliyo salama na viwanda vyetu vinapata malighafi safi na kupunguza uingizaji maziwa toka nje ya nchi,”.
Aidha amesema,kiasi kinachozalishwa kwa takwimu za mwaka 2025/2026 lita bil.4 na asilimia 5 ya maziwa yanayosindikwa,hivyo kiasi hicho ni kidogo ukilinganishwa na maziwa yanayozalishwa na kusema kuwa mahitaji halisi kwa nchi ni lita bil.13 .
Mratibu wa Taifa wa Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabianchi, Lazaro Kapera amesema,mradi huo unatekelezwa katika mikoa 12 hapa nchini, ukiwa na lengo la kuimarisha uzalishaji wa maziwa na kuongeza tija kwa wafugaji.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi huo mkoani Mbeya, Samora Mshang’a, amewataka wafugaji kutumia fursa zinazotolewa na mradi huo kuboresha ufugaji na kuongeza uzalishaji wa maziwa ili kutimiza matarajio ya Serikali.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Erica Yegela amesema,halmashauri hiyo imeendelea kuwawezesha wananchi, hususani wanawake kupitia mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani.
Amesema,hadi sasa zaidi ya sh.bil.2 zimetolewa kwa wanawake, hivyo halmashauri imeupokea mradi huo kwa mikono miwili kutokana na fursa unaotoa kwa wafugaji na wananchi kwa ujumla.
Mmoja wa wananchi wa kijiji cha Ihombe Yohana Syeu amesema,changamoto wanazokabiliana nazo ni pamoja na kufuga ng’ombe wasio na uwezo mkubwa wa kuzalisha maziwa, hali inayochangia uzalishaji mdogo.


More Stories
Yanga yatwaa Ngao ya Jamii ,Simba chali
Msajili wa Hazina, Fitch Ratings watathmini mageuzi ya taasisi za ummaNa Mwandishi wa OTRDar es Salaam
MNH-Mloganzila kufanya kambi ya upandikizaji figo na urekebishaji wa mishipa ya kuchuja damu