May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wafanyabiashara kukutana na kujadili changamoto wanazokabiliwa nazo

Na Penina Malundo,TimesMajira Online, Dar

MWENYEKITI wa Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC) Mercy Silla amesema ni muhimu wafanyabiashara kukutana na kujadili masuala ya biashara na changamoto wanazokabiliana nazo katika biashara zao.

Pia amesema miongoni mwa changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wengi ni pamoja na ukosekanaji wa masoko ya uhakika ambapo wafanyabiashara wengi wanajikuta kuvunjika moyo katika biashara zao.

Ameyasema hayo wakati wa mahojiano maalum na waandishi wa habari wakati wa mikutano ya ana kwa ana iliyoandaliwa na Tantrade kwenye maonesho ya Sabasaba Jijini Dar es Salaam mkutano uliokuwa umekutanisha wadau mbalimbali wa Sekta ya nafaka hapa nchi na nje ya nchi.

Amesema zipo changamoto zinazowakabili wadau wa nafaka na kubwa zaidi ni namna wanavyoweza kupata soko la bidhaa zao ambapo imefikia wakati wadau hao kukata tamaa.

Silla amesema wao kama TWCC wamekuwa na msaada Mkubwa kwa wafanyabiashara katika kuhakikisha wajasiriamali mbalimbali wakiwemo wa nafaka wanapata masoko ili kuuza bidhaa zao.

“Ndio maana hapa nimeweza kuwasilisha mada na mchango wetu kama TWCC ili kwa pamoja tuweze kuona namna gani wadau wa nafaka wanaweza kulifikia soko kwani soko lipo ndani na hata nje pia” amesema Silla.

Aidha ameipongeza Mamlaka ya Tantrade kwa kuendesha mikutano hiyo ya wafanyabiashara ya ana kwa ana kwa ufanisi mkubwa huku akisisitiza wananchi kujitokeza kwa wingi katika Banda la TWCC kujionea Bidhaa mbalimbali zenye ubora wa hali ya juu zinazozalishwa na wakina Mama wa TWCC kote nchini.

“kimsingi maonesho hadi kufikia leo yanakwenda vizuri na kama mnavyoona hapa kumechangamka na kikubwa wanawake wamejitokeza sana katika maionesho haya jambo ambalo linaleta faraja hususani kwenye Sekta ya Biashara hapa nchini” amesema Mercy.

Katika mkutano huo ambao pia ulifanyika kwa njià ya Mtandao ili kutoa fursa kwa wadau wengine walio mikoani na nje ya nchi kushiriki Mwenyekiti huyo aliiwakilisha Taasisi yake na kueleza changamoto mbalimbali zinazowakabili wadau wa nafaka nchini kupata soko la uhakika wa Bidhaa zao.