May 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wawekezaji vitalu vya NARCO watakiwa kufuata taratibu za mikataba

Na Elibariki Mafole, TimesMajira Online, Kagera

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Mashauri Ndaki amewataka wawekezaji kwenye vitalu vya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kufuata taratibu zilizowekwa kulingana na mikataba yao.

Ndaki ameyasema hayo juzi wilayani Misenyi Mkoa wa Kagera wakati alipotembelea Ranchi ya Mabale na kuzungumza na baadhi ya wawekezaji wenye mifugo katika vitalu hivyo.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (Mb) akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi kutoka wizarani na wawekezaji wa vitalu mara baada ya kumalizika kwa kikao kilichofanyika kwenye moja ya kitalu katika Ranchi ya Mabale wilayani Misenyi Mkoa wa Kagera.

Waziri Ndaki amesema kumekuwepo na tabia ya baadhi ya wawekezaji kuchukua vitalu na kutovitumia kama ilivyoelekezwa kwenye mikataba kitu ambacho kinasababisha maeneo kuwa mapori na kuvamiwa na watumiaji wengine wa ardhi.

Wizara kupitia NARCO imejipanga kuhakikisha wafugaji wanapata maeneo ya vitalu kwa ajili ya kufugia kitu ambacho kitasaidia kuondokana na tatizo la malisho na kupunguza migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na watumiaji wengine.

“Hivyo wizara kwa sasa imejipanga kuhakikisha wawekezaji katika vitalu wanatumia maeneo hayo kwa malengo yaliyokusudiwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanalipa kodi kwa wakati,” alisema Waziri Ndaki.

Vilevile alisema kuwa wizara kwa sasa inaiona NARCO kama ni sehemu ya kotokea kwani kupitia kampuni hiyo wizara itaweza kuongeza ukusanyaji wa mapato na kuongeza kipato wa wafugaji.

Akiwa katika Ranchi hiyo Waziri Ndaki amemtaka mwekezaji wa Kampuni ya Chobo Investment kuachia eneo analolimiliki kwa sasa wakati akiendelea kujipanga ili wawekezaji wengine ambao tayari wanayo mifugo waweze kulitumia. Aidha, amemuhakikishia mwekezaji huyo kuwa atapewa eneo kwenye Ranchi nyingine ikiwa atafuata masharti ya mkataba wa NARCO.

Vilevile kutokana na changamoto iliyoibuliwa kuhusu muda mfupi wa ukodishaji vitalu, Waziri Ndaki amewaagiza NARCO kuangalia uwezekano wa kuongeza muda wa mikataba ya muda mfupi ili iwe ni ya miaka mitano badala ya mwaka mmoja wa sasa.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayesimamia sekta ya Mifugo, Prof. Elisante Ole Gabriel amesema wizara imejipanga kuhakisha uzalishaji wa Mifugo na mazao yake unaongezeka na kuhakikisha wawekezaji katika sekta wanasaidiwa ili wasikwame katika uwekezaji wao.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Misenyi, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Abdallah Mayomba amesema kuwa uwepo wa Ranchi katika Wilaya hiyo umesaidia sana kupunguza migogoro ya ardhi lakini pia imesaidia kupunguza tatizo la malisho ambalo lilikuwa linawasumbua wafugaji.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wawezekaji hao wamemueleza waziri kuwa bado wanahitaji maeneo kwa ajili ya kufugia na kuwa wanaishukuru serikali kupitia NARCO kwa ajili ya kutenga maeneo hayo na kuwashushi gharama ya ukodishaji wa vitalu.