May 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi washauria kuacha kukunua ardhi kiholela

Na Judith Ferdinand,TimesMajira Online,Mwanza

WANANCHI wametakiwa kuacha kununua ardhi kiholela kwani kila kipande cha ardhi kimepangiwa matumizi pamoja na kujenga kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za ardhi na mipango miji.

Pindi wanapotaka kuendeleza maeneo yao hasa yale ya mijini ili kujiepusha na hasara zinazoweza kujitokeza ikiwemo kuvunjiwa nyumba zao kwa kutozingatia matumizi sahihi ya ardhi ya eneo husika.

Hayo yamezungumzwa na Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt. Angeline Mabula wakati akizungumza na wananchi wa Kata za Kahama na Kiseke ikiwa ni muendelezo wa ziara yake aliyoianza mwanzoni mwa wiki.

Ambapo ziara hiyo ni kwaajili ya kusikiliza kero za wananchi kuhamasisha utekelezaji wa shughuli za maendeleo, kukumbusha juu ya uchukuaji wa tahadhari dhidi ya Covid-19 na kutoa mrejesho wa vikao vya Bunge la bajeti lililoisha hivi karibuni.

Dkt.Angelina amesema,wananchi wanatakiwa kuhakikisha kabla ya kununua eneo na kulifanyia maendelezo kujiridhisha na matumizi sahihi ya ardhi ya eneo hilo kwa kushirikisha ofisi za ardhi za majiji na manispaa za eneo husika, viongozi wa maeneo yao, majirani wa pande zote ili kupunguza migogoro isiyokuwa ya lazima na hasara kwa kuingia gharama zisizo na umuhimu.

Amesema, wananchi wanapaswa kuacha kununua ardhi kiholela kwani kila kipande cha ardhi kimepangiwa matumizi yake.

Pia amesema,ni marufuku kujenga kiholela katika maeneo yote ya manispaa kwasababu yalishatangazwa kama maeneo ya miji hivyo huwezi kufanya uendelezaji wowote bila kuwa na kibali, ramani na kuhusisha ofisi zinazohusika.

Sanjari na hayo alitumia fursa hiyo aliahidi kutoa matofali yote yatakayohitajika katika ujenzi wa shule mpya ya msingi mtaa wa Isela.

Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Masala,Ofisa Tarafa wa wilaya hiyo Godfrey Mzava alimhakikishia ulinzi na usalama ndani ya wilaya hiyo huku akiwataka wananchi kutoa taarifa juu ya vitendo vya kiharifu na kushiriki utekelezaji wa miradi ya maendeleo

Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, Ofisa Ardhi na Mipango Miji wa Ilemela Shukran Kyando,alikemea vitendo vya matumizi ya ardhi bila vibali vya manispaa ikiwemo kuendesha biashara ya ufyatuaji wa matofali katikati ya makazi ya watu jambo linalochangia uharibifu wa mazingira kwa kuzalisha kelele.

Mmoja wa wananchi walioshiriki mkutano huo Hawa Kiboto mbali na kumpongeza Mbunge Dkt Angeline Mabula kwa ziara hiyo ameomba usimamizi zaidi wa sera ya afya inayotaka mama wajawazito na watoto wa chini ya miaka mitano kuhudumiwa bila gharama pindi wanapohitaji huduma ili kuokoa maisha ya mama na mtoto pindi inapojitokeza dharura.