March 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wadau wakutana kujadili na kuweka mikakati ya kunusuru watoto mitaani,ombaomba

Na Joyce Kasiki,timesmajira,Dodoma

WADAU mbalimbali wamekutana jijini Dodoma kujadili na kuweka mikakati thabiti ya kukabiliana na changamoto ya uwepo wa watoto wa mitaani,ombaomba na wanaoishi katika mazingira hatarishi kwa lengo la kupungiza kama siyo kumaliza kabisa changmoto hiyo.

Akifungua Mkutano wa siku mbili wa wadau hao  kwa niaba ya Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt.Dorothy Gwajima ,Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Idara Kuu ya Mawndeleo ya Jamii Dkt.John Jingu amesema bado changamoto ya watoto hao kubwa na lazima kuwepo na mkakati thabiti wa kuitatua na kwamba , takwimu mbalimbali zinaonyesha hali halisi ya ukubwa wa tatizo hilo.

“Nchi yetu inakabiliwa  na tatizo la kuwa na watoto wa mitaani na kwa takwimu zilizopo ni kwamba nchi yetu  inakadiriwa kuwa na  idadi ya watoto 35,919 wanaoishi na kufanya kazi mitaani katika majiji na miji mbalimbali hapa nchini (Taarifa ya TAMISEMI, 2018). ” amesema na kuongeza kuwa

“Tafiti mbalimbali zimefanyika ili kubaini hali halisi ya watoto hawa mathalani “Head Count Survery” ya mwaka 2017 katika mikoa ya Mwanza, Dodoma, Arusha, Mbeya, Iringa na Dar es salaam ilibaini jumla ya watoto 6,393 ambao walikuwa wanaishi na kufanya kazi mtaani. Zaidi ya asilimia 90 ya watoto hao wazazi/walezi wao wanafahamika wanapoishi. “

Dkt.Jingu amesema “kwa msingi huu tumeona ni vyema kuwa na kikao hiki chenye wadau muhimu ili tuweze kujadili na kuwa na mkakati wa pamoja unaolenga kuondoa changamoto hii,na ni imani yangu kikao hiki kitatoka na mkakati utakao tusaidia kutatua changamoto hii kwa maslahi mapana ya watoto wetu na Taifa kwa ujumla.”

Aidha amesema kundi la watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani liko katika hatari ya kutumikishwa katika magenge yasiyofaa ya kihalifu na kwamba ni vyema kundi hilo liangaliwe kwa jicho pana na la kipekee kwani kwa kufanya hivyo itasaidia  kuwaokoa watoto hao kwa faida yao wenyewe, kwa familia zao na Taifa zima kwa ujumla. 

“Kikao hiki  ni cha muhimu sana kwetu kwani kitatusaidia kujadili na kuwa na mkakati wa  pamoja wa  namna bora ya kuondokana na changamoto hii.” Amesisitiza

Kwa mujibu wa Dkt.Jingu amesema lengo kuu la kuwa na mkakati wa pamoja ni kuwa na mtazamo wa pamoja unaounganisha  nguvu kwa lengo la kumaliza kama siyo kupunguza changamoto hiyo huku akiwataka wajumbe wa mkutano huo kuhakikisha  wanaandaa mkakati unaotekelezeka na kuwa na tija kwa vizazi vijavyo.

Aidha ameagiza kufanyika zoezi la utambuzi wa watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani na omba omba  katika mikoa yote pamoja na kuhakikisha kuwa watoto hao wanarejeshwa katika jamii zao .

Vile vile ameagiza Elimu itolewe kwa jamiii ili waepukane na kutoa fedha kwa ombaomba kwani  inahamasisha ombaomba wakiwemo watoto kuwepo mitaani,elimu sahihi ya malezi kwa familia na jamii na kuondoa mila potofu zinazochangia kuongezeka kwa matendo ya ukatili ambayo hupelekea watoto kukimbilia mtaani lakini pia Mamlaka za Serikali za Mitaa zitunge Sheria ndogo kwa ajili ya kusimamia afua za kudhibiti suala la watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani pamoja na ombaomba.

Pia ameziagiza halmashauri kusimamia wadau na kuwaelekeza badala ya kuwapatia misaada watoto wakiwa mitaani, waelekeze huduma na misaada kwenye familia na makao ya watoto.

Vile vile Dkt.Gwajima ameziagiza Serikali ngazi za vijiji/mitaa  kusimamia familia ili wazazi/walezi waweze  kutoa malezi sahihi,kuimarisha  uratibu kupitia  kamati za MTAKUWWA,kuwatambua na kuwaunganisha watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani na mafunzo ya ufundi stadi kama sehemu ya marekebisho ya tabia na kujenga stadi za maisha.

Amesema,watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani ni moja ya makundi ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi yaliyoainishwa katika Sheria ya Mtoto Na. 21 ya 2009 na kufanyiwa marekebisho mwaka 2019.

“Aidha, kutokana na mazingira wanayoishi hujikuta katika hatari ya kukumbana na changamoto mbali mbali ikiwemo kuingia katika mkinzano na sheria kutokana na kutokuwa na uangalizi  madhubuti na uhakika wa kupata mahitaji muhimu kama vile chakula, mavazi, malazi na afya.

Pia amesema,wapo wengine wanaokumbana na vitendo vya ukatili vikiwemo kubakwa na kulawitiwa. Pia miongoni mwa watoto hawa wapo wanaingia katika kundi la ombaomba ambapo hutumia fedha wanazopata kujikimu mahitaji yao.

Naye Kaimu Kamishna wa Ustawi wa Jamii Shilungu Ndaki akiwasilisha taarifa ya Hali ya tatizo hilo nchini amesema Serikali imefanya jitihada mbalimbali zinazolenga kuzuia ongezeko la watoto hawa na pia kutoa huduma ya msaada kwa watoto ambao wako tayari mtaani.

Ametaja miongoni mwa jitihada hizo ni pamoja na kusimamia Kamati za Mpango wa Taifa wa Kutokomeza ukatili kwa Wanawake na Watoto (MTAKUWWA), kusimamia programu zinazolenga uchumi wa kaya na kutengeneza muongozo wa kuunganisha watoto na familia.

Ndaki amesema kwamba hadi mwezi Machi mwaka huu watoto 1005 waliokuwa mitaani wameunganishwa na wazazi wao hivyo kupunguza watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani katika miji na majiji.

“Changamoto kubwa pamoja na jitihada hizo watoto wameendelea kuongezeka hasa kutokana wazazi kutotimiza majukumu yao, migogoro ya ndoa na kuongezeka kwa vitendo vya ukatili kwenye familia”. ameongeza Ndaki.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la PACT Tanzania Mariana Balampama amesema kuwa, suluhisho la kudumu linahitaji ushirikiano mkubwa wa sekta mbalimbali ikiwemo kuwa na mikakati madhubuti zaidi kuzuia tatizo hilo na kubuni mbinu endelevu kwa watoto hao kwani ni sehemu muhimu kwa kizazi kijacho.