September 26, 2021

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Balozi wa Marekani aipongeza Muhimbili

Na Mwandishi wetu,timesmajira,Online

BALOZI  wa Marekani nchini Tanzania, Donald Wright ameipongeza Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa kutoa huduma za ubingwa wa juu baada ya kutembelea Idara ya Magonjwa ya Dharura na Idara ya Afya ya Magonjwa ya Akili.

Akizungumza katika ziara hiyo baada ya kutembelea Hospitali hiyo,Balozi Wright amesema ameshuhudia jinsi wataalamu wanavyotoa tiba kwa wagonjwa wa magonjwa ya dharura wanaofikishwa katika idara ya magonjwa ya dharura.

Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa Muhimbili, Dkt. Hedwiga Swai amemweleza Balozi Wright kwamba hospitali imekuwa ikipokea wagonjwa kutoka mikoa mbalimbali nchini na kuwapatia matibabu ingawa ya kuwepo kwa upungufu wa wataalamu wa afya.

“Pamoja na Hospitali kuwa na upungufu wa wataalamu wa afya, tumekuwa tukipambana kutoa huduma bora za ubingwa wa juu kwa wagonjwa wote wanaofika Muhimbili,” amesema Dkt. Swai.

Naye Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura wa Muhimbili, Dkt. Juma Mfinanga amesema idara hiyo imekuwa ikipokea wagonjwa 200 hadi 300 kwa siku kutoka maeneo mbalimbali ya nchi pamoja na nje ya nchi.

Amesema idara hiyo inatoa huduma za dharura pamoja na kufundisha wataalamu mbalimbali wanaotoa huduma za dharura nchini na nje ya nchi.

Huku Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Afya ya Akili, Dkt. Jessie Mbwambo alimweleza balozi huyo jinsi idara hiyo ilivyofanikiwa kutoa huduma kwa wagonjwa wa afya ya akili nchini.

Katika Idara ya Magonjwa ya Afya ya Akili, baadhi ya watu waliotibiwa kwa muda mrefu walitoa ushuhuda jinsi walivyopona na sasa wanaendelea na shughuli zao kama kawaida.  

Balozi Wright amefanya ziara katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS), Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) na Taasisi ya Moyo  Jakaya Kikwete (JKCI) ambako ameelezwa jinsi tafiti za kudhibiti magonjwa  mbalimbali zilivyofanyika. Utafiti huo umejumuisha magonjwa ya afya ya akili, malaria, kifua kikuu, ajali na magonjwa yasioambukiza