May 27, 2022

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

‘Waandishi wa habari endeleeni kuibua habari za wenye ulemavu’

Na Esther Macha,timesmajira,online, Mbeya

MKURUGENZI Huduma kwa Watu wenye Ulemavu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Jacob Mwinula, amewataka waandishi wa habarini nchini kuendelea kuibua changamoto za watu wenye ulemavu waliopo mijini na vijijini kwa kuhakikisha changamoto hizo haziwadhalilishi watu hao.

Mwinula alisema hayo jana wakati wa kikao cha siku mbili cha waandishi wa habari ,Serikali kuhusu watu wenye ulemavu kwa njia ya mtandao .

Hata hivyo, alisema kuwa ofisi ya waziri Mkuu ipo tayari kuendelea kuwasaidia watu wenye ulemavu na kuwapa ushirikiano mkubwa katika masuala mbali mbali yanayowazunguka katika jamii .

“Nduguwaandishi wa habari endeleeni kutoa taarifa za watu wenye ulemavu  pamoja na kutoa taarifa sahihi waliopo mijini na vijijini kikubwa wasidhalilishwe,” alisema.

Kwa upande wake Mratibu wa Mradi kutoka Internews, Shaban Maganga alisema waandishi wa habari waliofanya vizuri katika kuandika habari za watu wenye ulemavu watapata fursa ya kushiriki mikutano ya kimataifa.

Hata hivyo, Maganga aliwapongeza waandishi wa habari kwa kazi nzuri ambazo wanaendelea kuzifanya za kuhabarisha jamii kuhusu masuala ya watu wenye ulemavu na kwamba Internews itaendelea kuunga mkono jitihada za waandishi wa habari katika kuripoti masuala ya walemavu.

Kwa upande wake Josephine Lyengi kutoka ofisi ya Waziri Mkuu alisema umaskini umezidisha unyapaa kwa watu wenye ulemavu kutokana na jamii au familia kuwaona watu wa tofauti .

Naye Mkufunzi na Ofisa Mkuu wa Miradi kutoka Taasisi ya Vijana wenye Ulemavu (YOWDO),Genarius Gaisha alisema vema kuzingatia lugha za matamshi kwa watu wenye ulemavu na kuomba jamii kuondokana na tamadani  za zamani  kuwa watu wenye ulemavu ni watu wasiojiweza.

“Tutambue kuwa watu wenye ulemavu wana mahitaji,  wanahiraji kuheshimiwqa  kama watu wengine kwenye jamii ,tukitumia lugha nzuri tunaweza kuondoa unyapaa kwa watu wenye ulemavu “alisema Gaisha.