May 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mtendaji Mkuu wa OSHA ,Khadija Mwenda akiwa na mkurugenzi wa usalama na Afya toka OSHA Mhandisi Alex Ngata katika kikao kazi mkoani Morogoro.

Waajiri watakiwa kuelewa dhana ya Usalama mahali pa Kazi

Na Bakari Lulela,TimesMajira,Online

MWENYEKITI wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Usalama na Afya Mahala Pa kazi (OSHA) Dkt. Adelhem Meru amewashauri waajiri nchini kuielewa vizuri dhana ya usalama na afya mahali pa kazi na hivyo kuhakikisha wanalinda afya na usalama  wa wafanyakazi wao ili waweze kuzalisha kwa wingi na kufikia malengo waliojiwekea.

Kauli hiyo imetolewa mjini Morogoro wakati wa kikao kazi baina ya wakala wa Usalama na Afya Mahala Pakazi (OSHA) pamoja na Chama cha Wafanyabiashara,Viwanda na Kilimo Nchini (TCCIA) mkoani Morogoro kwenye kikao kazi ambacho pia kilikuwa na lengo la kuitambulisha kampeni ya vision zero mkoani humo.

 kampeni maalumu ambayo inalenga kupunguza ajali na magonjwa sehemu za kazi.

Dkt. Meru amesema endapo waajiri hawatazingatia masuala ya usalama na afya hawataweza kufikia malengo yao waliojiwekea ambao ni lengo kubwa la mfanyabiashara kuhakikisha kuzalisha bidhaa za kutosha.

“Usalama na Afya mahali pakazi ni nguzo muhimu katika uzalishaji katika utoaji wa huduma mahali popote pale ukiwa na wafanyakazi ambao afya zao sio bora uzalishaji wao utakuwa sio bora matokeo yake hata malengo kama mwajiri waliojiwekea yatakuwa sio bora,”amesema na kuongeza

“Nawahamasisha waajiri wote kuielewa vizuri dhana ya usalama na afya kiuhalisia tukitoka hapa tuende kuwahamasisha wafanyakazi wetu wanakuwa katika mazingira ambayo si salama na sio dhaifu,” amesema Dkt. Meru

Dkt. Meru amepongeza juhudi za Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuweza kuifikisha nchi kwenye uchumi wa kati hata kabla ya muda ambao ulikuwa umepangwa.

Amesema  sera za nchi zilikuwa zinasema nchi itafikia uchumi wa kati ifikapo 2020/2025  kutokana na uongozi shupavu wa Rais Magufuli amewezesha kufikia uchumi wa kati hata kabla ya muda uliopangwa.

Kaimu  Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pakazi, Khadija Mwenda amesema waliona kuna umuhimu OSHA kushirikiana na TCCIA katika kuhamasisha wanashughulikia kero na changamoto za wafanyabiashara nchini,kwani mchango wao ni mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi.

Mwenda amesema kuwa OSHA kama taasisi wezeshi itaendelea kushirikiana na wadau kupitia vyama vyao ili kuweza kutatua changamoto zinazowakabili,alisema sekta ambayo sio rasmi inayoajiri watu wengi sana hivyo wataendelea kushirikiana na TCCIA  katika kuhakikisha sekta hii inaendelea katika ukuaji wa uchumi.

Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Morogoro Mwadhini Myanza amesema kwa kuishukuru OSHA kwa kutekeleza ipasavyo yale yote yaliyotekelezwa kwenye Blue print na hivyo kuwasaidia wadau wao.

“OSHA ni chombo ambacho huwezi kukiweka pembeni katika mapinduzi ya viwanda kwa sababu kila mahali unapopiga hatua unahitaji kuwa na elimu ya usalama na afya wakati wa uzalishaji, kwa hotuba hii imetuzindua na kukumbuka kuwa serikali yetu imefanya mambo mengi kwa sababu mambo yote ambayo yaliyotolewa kwenye Blue print OSHA imejitahidi kuzingatia ushauri uliotolewa sasa tunaenda vizuri,” amesema Myanza