May 21, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Viongozi wa dini,serikali za mitaa na watu wa Madawati ya kijinsia watakiwa kusaidia jamii inayokumbwa na ukatili wa kijinsia

Na Penina Malundo,timesmajira,Online

WITO umetolewa kwa Viongozi wa dini,Serikali za mitaa pamoja na watu wa madawati ya kijinsia kuisaidia a jamii inayokabiliana na hali ya ukatili wa kijinsia husasani wanawake na watoto.

Akizungumza hayo juzi  katika Mkutano uliowahusisha viongozi hao mkoani Dar es Salaam,Mwenyekiti  wa Taasisi ya Women Tapo Tanzania ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Tabata Women Tapo,Stella Mbaga   amesema lengo la mkutano huo ni kuendelea kuwasaidia wakinamama wanapopata changamoto za ukatili wa kijinsia katika nyumba zao kujua wapi wanaweza kupata msaada.

Amesema mara kwa mara shirika lao limekuwa likiwakutanisha wamama wakiwemo wale wanaofanya shuguli zao sokoni na wachuuzi na kuwaelimisha juu ya masuala mbalimbali ikiwemo suala la kutofumbia macho  ukatili wa kijinsia wanaokumbana nao majumbani au masokoni kwa lengo la kuhakikisha wanaripoti sehemu sahihi.

“Shirika letu ni miongoni mwa mashirika ambayo yanajishughulisha na uelimishaji  wa wakinamama wa masoko,wasichana na watoto kujua haki zao mbalimbali,”amesema na kuongeza

“Haya Matapo yapo mengi nchini ,ila sisi TAPO letu ni la Tabata imekuwa ikitoa elimu mbalimbali ikiwemo Jinsia,Afya na fedha na imekuwa msaada mkubwa kwa wamama wa Tabata na kusaidia kwa kiasi kikubwa wamama kujisimamia hata pale wanapotewkelekezwa na wanaume zao,”amesema

Aidha amesema  mkutano huo umekuja kuwasaidia viongozi wa serikali za mitaa,viongozi wa dini na watu wa madawati ya kijinsia  kuelewa suala zima la ukatili wa kijinsia.

Mtoa Mada ya masuala ya ukatili wa kijinsia Jema Akilimari akitoa mada kwa wadau mbalimbali waliojitokeza katika semina ya ukatili wa kijinsia.

Amesema viongozi hao watakapoelewa dhana nzima ya ukatili wa kijinsia itaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa wamama wanapoenda kutoa taarifa za hali hiyo inapowatokea viongozi hao wajue wanawasaidiaje.

“Mkutano wa leo utakuwa chachu kubwa kuwafungua juu ya matatizo hayo ya ukatili wa kijinsia ikiwemo ukatili wa  kulawiti Watoto ambao kwa sasa umekuwa ukishika kasi,”amesema

Kwa Upande wake Mwinjilisti wa Kanisa la Kiinjilisti la Kiluteli (KKKT)ushirika wa Tabata Shule ,REV. Richard Kibwana  amesema ni vema suala la ukatili wa kijinsia kuendelea kufundishwa katika jamii ili watu waepuke ukatili wa kijinsia kwani  ni jambo baya.

“Tunaona ni namna gani kesi za ukatili zinavyofika Kanisani au wakati mwingine Misikitini na unakuta ukatili wanaweza kufanyiwa wanawake au ndugu, kwa kweli ukatili unaofanywa haya  Mungu uwa hapendezwi nao,”amesema

Amesisitiza kuwa kama wazazi ,viongozi wa dini,viongozi wa serikali wanapaswa kukemea kwa pamoja juu ya ukatili wowote  ikiwemo kipigo,kunyimwa haki za msingi, na ukatili wanaofanyiwa watoto kukosa haki zao za msingi.