Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
UFADHILI unaotolewa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) umeendelea kuleta matokeo chanya katika kuongeza uzalishaji wa mazao na bidhaa za kilimo, huku ukiimarisha viwanda vya usindikaji na kuongeza soko la mazao ya wakulima nchini.
Mafanikio hayo yalielezwa leo Agosti 3,2026 katika Maonesho ya 33 ya NaneNane wakati Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Emmanuel Nchimbi, alipotembelea banda la TADB na kupokea taarifa kuhusu mchango wa benki hiyo katika kukuza uzalishaji wa kilimo na kuimarisha mnyororo wa thamani wa mazao.
Akiwa ameambatana na Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, Makamu wa Rais alipokea maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Mipango, Ushauri na Mahusiano ya Taasisi wa TADB, Mkani Waziri,ambapo amesema Benki hiyo imeendelea kutoa mikopo na huduma za kifedha kwa wakulima, wafugaji, wavuvi na wawekezaji wa sekta ya kilimo ili kuongeza uzalishaji, tija na kuimarisha usalama wa chakula.
Akitoa ushuhuda wa matokeo ya ufadhili huo, Mkurugenzi wa Kiwanda cha Mafuta ya Kula cha Trolle Meesle, Daniel Amulike,amesema uzalishaji wa mafuta ya kula umeongezeka kutoka tani 30 hadi tani 624 kwa mwezi baada ya kupata ufadhili wa TADB, hatua iliyoongeza uwezo wa kununua mazao kutoka kwa wakulima na kupunguza utegemezi wa mafuta yanayoagizwa kutoka nje ya nchi.
Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo,amesema Serikali itaendelea kuimarisha uzalishaji wa mazao ya mafuta na kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya uchakataji, akieleza kuwa ushirikiano na taasisi za kifedha kama TADB ni muhimu katika kuongeza thamani ya mazao na kukuza uchumi wa kilimo.

More Stories
DCEA yateketeza hekari 3,117.9 mashamba ya bangi Lindi
Watakiwa kuwajengea uwezo wakulima kunufaika na masoko ya nje
Tanzania yampokea Mr Alaya, mhamasishaji wa Amani