Na.Mwandishi wetu,Timesmajira
Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na Tanzania Safari Channel, imemkaribisha rasmi nchini Tanzania mhamasishaji wa amani duniani na mpiga hatua wa kimataifa, Saddam Suleiman Ali Alaya, anayetekeleza safari ya kihistoria ya The World’s Longest Peace Walk.
Saddam ameingia nchini kupitia Mpaka wa Kasesya uliopo Wilaya ya Kalambo, mkoani Rukwa, akianzia rasmi hatua ya safari yake ya takribani siku 35 nchini Tanzania.
Katika kipindi hicho atapita katika mikoa ya Rukwa, Katavi na Kigoma kabla ya kuondoka kupitia Mpaka wa Manyovu, akiwa na dhamira ya kuhamasisha amani, mshikamano wa kimataifa na kuitangaza Tanzania kama moja ya vivutio bora vya utalii duniani.

Safari hii ni sehemu ya mradi wa kimataifa unaolenga kutembea zaidi ya kilomita 23,000 kutoka Cape Town, Afrika Kusini hadi Magadan, Urusi, kupitia nchi 18 kati ya mwaka 2026 na 2028.
Tanzania ni nchi ya tano katika historia ya safari hiyo, jambo linaloipa fursa ya kipekee ya kuonesha urithi wake wa asili, utamaduni na ukarimu kwa hadhira ya kimataifa.
Kwa mujibu wa waratibu wa mradi huo, safari inaungwa mkono na kampeni kubwa ya kimataifa ya vyombo vya habari, utengenezaji wa makala maalumu na ushirikiano na mitandao mbalimbali ya kimataifa inayotarajiwa kufikia zaidi ya watu milioni 480 duniani, huku pia ikilenga kuweka rekodi saba za Guinness World Records.

Kupitia ushirikiano huu, Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia TTB inaendelea kutumia majukwaa ya kimataifa kuitangaza Tanzania kama kitovu cha utalii, amani na urithi wa dunia, huku ikiwakaribisha wageni kutoka kila pembe ya dunia kutembelea vivutio vya kipekee vya nchi.



More Stories
DCEA yateketeza hekari 3,117.9 mashamba ya bangi Lindi
Watakiwa kuwajengea uwezo wakulima kunufaika na masoko ya nje
Ufadhili wa TADB waimarisha Viwanda vya Kilimo