Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
CHUO cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kimesema kinaimarisha tafiti na programu za mafunzo ili kuongeza idadi ya marubani na wahandisi wa matengenezo ya ndege nchini, hatua inayolenga kukidhi mahitaji yanayoongezeka katika sekta ya usafiri wa anga.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa leo Agosti 3,2026 na Mkuu wa NIT, Dkt. Prosper Mgaya,amesema tafiti za Chuo zimebaini kuwa Tanzania bado inakabiliwa na upungufu mkubwa wa wataalamu hao, hali inayozifanya baadhi ya kampuni za ndege kutegemea wataalamu kutoka nje ya nchi.

Amesema ongezeko la uwekezaji wa Serikali katika Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), ikiwemo ununuzi wa ndege 16 za kisasa, limeongeza hitaji la kuwa na wataalamu wa kutosha watakaohakikisha ndege zinaendelea kutoa huduma kwa ufanisi bila kusimama kutokana na ukosefu wa marubani au wahandisi.
Mgaya ameeleza kuwa kupitia mafunzo yenye viwango vya kimataifa, NIT inalenga kuwaandaa Watanzania wenye ujuzi wa kitaalamu ili kupunguza utegemezi wa wataalamu wa kigeni, kuokoa fedha zinazotumika kuwaajiri na wakati huohuo kuongeza ajira kwa vijana katika sekta ya usafiri wa anga.
Kwa upande wake Mwanafunzi wa NIT,Catherine Ephraim ameeleza maono yake katika Sekta ya Uhandisi wa Ndege ambapo amesema dhamira yake ni kuwa Mhandisi mahiri wa matengenezo ya ndege ili kuchangia katika usalama na maendeleo ya sekta hiyo nchini na kimataifa.

Ephraim amesema anataka kuwa Mhandisi mwenye uwezo, ustadi, na uledi wa hali ya juu utakaohakikisha sekta ya usafiri wa anga nchini Tanzania inazidi kuimarika na kudumu.
“Najivunia kusema kuwa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) ndio msingi unaonifanya niwe karibu na kutimiza maono haya. Tunapata elimu bora, mafunzo ya vitendo, pamoja na uongozi wa wakufunzi wenye uzofu wa kutosha wanaotufundisha na kutuelekeza,”amesema Ephraim.
Aidha mwanafunzi huyo alitumia fursa hiyo,kuwahimiza vijana wote nchini Tanzania hususani wasichana kutokuogopa na kujitokeza kwa wingi kujiunga na kozi ya Uhandisi wa Matengenezo ya Ndege, akibainisha kuwa kozi hiyo inawezekana na ada yake ipo katika kiwango kinachohimilika.
Naye Mwanafunzi wa fani ya urubani katika Chuo hicho katika ngazi ya PPL,Paulo Kabunda,amesema imekuwa ni ndoto yake kusomea fani ya urubani tangu akiwa mtoto mdogo.

“Na mpaka kufikia hivi sasa, naishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kwa kuweza kuturahisishia na kutusogezea karibu masomo haya ya urubani hapa hapa Tanzania na kwa bei ambayo hata sisi watanzania tunaweza tukamudu na tukasoma kwa ngazi kuanzia PPL mpaka kufikia leseni ya pili ya CPL,”amesema Kabunda.

More Stories
DCEA yateketeza hekari 3,117.9 mashamba ya bangi Lindi
Watakiwa kuwajengea uwezo wakulima kunufaika na masoko ya nje
Ufadhili wa TADB waimarisha Viwanda vya Kilimo