Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Licha ya jitihada zinazoendelea kufanyika nchini kuzuia ndoa za utotoni ili kuwapa wasichana nafasi ya kutimiza ndoto zao, bado changamoto kubwa ya uelewa wa sheria kuhusu umri sahihi wa kuolewa imeendelea kuwepo, hususan katika maeneo ya vijijini.
Kauli hiyo imetolewa leo Machi 28, jijini Dar es Salaam, katika kikao cha kitaifa cha viongozi wa dini kuhusu mabadiliko ya kisheria ya ndoa, na Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Sheikh Khamisi Mtaka.
Amesema kuwa katika mapambano dhidi ya ndoa za utotoni, kuna changamoto ya kutofautiana kati ya sheria za nchi, mafundisho ya dini na mitazamo ya kijamii, hali inayosababisha ugumu katika utekelezaji wake.
Ameeleza kuwa bado hakuna sheria madhubuti inayokataza moja kwa moja ndoa za utotoni, isipokuwa sera ya elimu ya mwaka 2014 inayokataza mwanafunzi kuolewa au kupata ujauzito akiwa shuleni.

“Endapo kipengele hiki kitaingizwa pia katika mifumo ya kijamii na kidini bila kukinzana, kitasaidia kuhakikisha anayetarajiwa kuolewa anakuwa amekomaa kiakili,” amesema Sheikh Mtaka.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwepo kwa sera na sheria zinazoainisha umri sahihi wa kuolewa kwa mtoto wa kike ili kulinda haki zao na kuwapa fursa ya kufikia malengo yao maishani.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Chuo cha Songea Catholic Institute of Technical Education, kilichopo Jimbo Kuu la Songea mkoani Ruvuma, Padri Longino Kamuhabwa amesema kuwa hata mafundisho ya dini yanasisitiza umuhimu wa mtu kuwa na ukomavu wa akili kabla ya kuingia kwenye ndoa.
Akinukuu Biblia (Mwanzo 1:27), amesema kuwa pamoja na agizo la kuzaa na kuongezeka, bado ndoa inahitaji maandalizi ya kisaikolojia na uwajibikaji wa hali ya juu.

“Ndoa inajengwa juu ya msingi wa upendo na uwajibikaji, hivyo ni muhimu kuhakikisha mhusika anakuwa na uhuru wa kufanya maamuzi na ukomavu wa kutosha,” amesema Padri Kamuhabwa.

Naye Afisa kutoka taasisi ya Msichana Initiative,amesema kuwa tafiti walizofanya katika mikoa mbalimbali zimebaini kuwa katika maeneo ya vijijini, ukosefu wa elimu pamoja na mila na desturi bado vinachangia kwa kiasi kikubwa kuendelea kwa ndoa za utotoni.

Naye Afisa Msichana Insiative Wakili Lucy Gidamis ameongeza kwa kusema kuwa jamii nyingi bado zinaweka mbele maslahi ya kiuchumi badala ya ustawi na haki za mtoto wa kike, jambo linalohitaji juhudi za pamoja kutoka kwa serikali, viongozi wa dini na wadau wa maendeleo ili kulitatua.

More Stories
Serikali yaongeza nguvu kwa wachimbaji wadogo,yasisitiza usalama Migodini
REA imeleta mageuzi sekta ya nishati
Mbega ataka viongozi kuimarisha ulinzi kudhibiti wageni