August 4, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vijana wa BBT watafuta fursa TADB

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dodoma

VIJANA wa Program ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) kutoka Samia Ndogowe AMCOS kutoka Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma wamekusanyika kwenye Banda la Nanenane la Benki ya Maendeleo ya kilimo (TADB) ili kusikia na kujifunza fursa mbalimbali za benki hiyo.

Moja ya fursa hizo ni pamoja na kupata elimu namna ya kujijenga kwenye miradi ya kiuchumi, kuendeleza miradi waliyoianzisha, na kuweza kupata mikopo na kuongeza mitaji yao kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao za kiuchumi ambazo tayari wanaendelea nazo.

“Vijana wa BBT wakiwa Banda la Benki ya TADB, Nanenane, Dodoma.”

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi Agosti 3, 2026 kwa nyakati tofauti kwenye Banda la Nanenane la Benki ya TADB katika Maonesho ya 33 ya Kilimo yanayofanyika kwenye Viwanja wa Dkt. John Malecela jijini Dodoma, vijana hao walisema kuna fursa nyingi zinatolewa na benki hiyo.

Kelvin Fezza amesema AMCOS yao inajishughulisha na kilimo biashara na mazao, lakini kabla ya kuja hapo kutafuta fursa, tayari Benki ya TADB siku za nyuma ilishawahi kuwasaidia vifaa kinga kwa kufanya kilimo kwa vitendo kama overall, vifaa vya kuzuia wakati wa kupulizia dawa, toroli na leki.

“Mimi ni mmoja wa wanufaika kwenye Shamba la Kilimo la BBT Samia Ndogowe AMCOS, tupo Wilaya ya Chamwino, Kijiji cha Ndogowe/Mlazo. Mimi kama kijana pamoja na vijana wenzangu ambao tupo chini ya AMCOS, chama kinachoshughulika na kilimo, mazao na masoko, tupo hapa Nanenane kwa ajili ya kupata semina na kujifunza ni namna gani Benki ya TADB inaweza kutunufaisha sisi kama vinana kuona namna gani tunaweza kujihusisha na kilimo, ama kwenye mnyororo mzima wa thamani wa kilimo.

“Vijana wa BBT wakiwa Banda la Benki ya TADB, Nanenane, Dodoma.”

“Moja ya manufaa ambayo tumewahi kuyapata kama vijana kupitia Mradi huu wa BBT tumeshawahi kupokea vifaa kinga kutoka Benki ya TADB kwa ajili ya kufanya kilimo kwa vitendo mfano kama ma- overall, vifaa vya kuzuia wakati wa kupulizia dawa, toroli, leki na chelewa. Lakini kwa vile bado tunaendelea tunapambana katika uzalishaji, tumekuja kuona ni namna gani TADB itaweza kutuwezesha mikopo sisi ili kujikita kwenye kilimo, hivyo tumekuja hapa kupata semina na kujua mambo mawili matatu tujue wapi pa kuingilia” amesema Fezza.

Naye Joyce Magita kutoka AMCOS hiyo, amesema wao kama vijana wanajishughulisha na kilimo cha alizeti pamoja na mbogamboga na kwa sasa wanalima tikitimaji, na kueleza nia iliyowapeleka Benki ya TADB.

“Kilichonileta TADB Bank ni kupata fursa ni kutokana na mimi nipo katika AMCOS, tunahitaji fursa kwa ajili ya mikopo. Tunajua Brnki ya TADB ni benki ya wakulima, na ni benki inayowasaidia wakulima wadogo wadogo kwa ajili ya kuwainua na kukuza mitaji yao midogo na kuwa mitaji mikubwa.

“Kelvin Fezza akizungumzia fursa za Benki ya TADB”

“Nimejifunza namna ya kukopa benki, namna ya kufanya mnyororo wa thamani ninapotoa mazao yangu shambani, hivyo nina uwezo wa kujiendeleza kwenye shughuli zote za kilimo”amesema Magita.

“Joyce Magita, akizungumzia fursa za Benki ya TADB.”
“Vijana wa BBT wakiwa Banda la Benki ya TADB, Nanenane, Dodoma.”