Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
CHUO Kikuu Mzumbe kimetekeleza jumla ya miradi 27 ya maendeleo yenye thamani ya takribani shilingi bilioni 15.66 katika mwaka wa fedha 2025/26, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya kufundishia, kujifunzia na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wanafunzi pamoja na watumishi katika kampasi zake zote.
Akizungumza na waandishi wa habari, jijini hapa leo Agosti 4,2026 kuhusu utekelezaji wa miradi ya mwaka 2025/26 na mwelekeo wa mwaka 2026/27 ,Profesa William Mwegoha Makamu Mkuu wa Chuo hicho amesema miradi iliyotekelezwa imehusisha ukamilishaji wa majengo ya taaluma na utawala, ujenzi wa studio ya kisasa ya multimedia, madarasa janja, ukarabati wa hosteli za wanafunzi, ujenzi wa vituo vya afya, maboresho ya miundombinu ya TEHAMA pamoja na ujenzi wa barabara za ndani na uwekaji wa taa za nishati ya jua.

Amesema Chuo hicho pia kimeongeza uwezo wa mtandao wa intaneti kutoka MBPS 650 hadi 1,140 katika kampasi zote tatu, huku kikinunua vifaa vya kisasa vya TEHAMA, magari ya viongozi, basi la wafanyakazi na lori la shughuli za ujenzi ili kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma.
Kwa mujibu wa Makamu Mkuu huyo, kupitia Mradi wa Higher Education for Economic Transformation (HEET), Chuo kinaendelea kujenga majengo ya mihadhara, hosteli, kituo cha TEHAMA, miundombinu ya maji na majitaka pamoja na kampasi mpya ya Tanga. Alisema uwekezaji huo utaongeza uwezo wa Chuo kudahili wanafunzi wengi zaidi na kuboresha ubora wa elimu ya juu nchini.
Aidha, Prof.Mwegoha amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2026/27 kinatarajia kutekeleza miradi mipya yenye thamani ya shilingi bilioni 4.83 kutoka fedha za ndani, sambamba na kukamilisha miradi inayoendelea kupitia mradi wa HEET na kuendelea kuwekeza katika tafiti, matumizi ya akili bandia (AI) na kuboresha huduma za TEHAMA.
Chuo pia kimeweka lengo la kuongeza idadi ya wanafunzi hadi 22,000 katika mwaka wa masomo 2026/27, huku kikiendelea kupanua miundombinu na vyanzo vya mapato kupitia uwekezaji katika mali na ardhi zake zilizopo katika mikoa mbalimbali nchini.


More Stories
Makatibu Wakuu wakutana kujadili mradi wa BRT
SCADA waimarisha udhibiti wa mafuta nchini
Vijana wa BBT watafuta fursa TADB