April 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwanaharakati Alexei Navalny. (Picha na WSJ)

Urusi yaandamwa sakata la Alexei Navalny kupewa sumu

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Dominic Raab amesema kuwa, Urusi lazima ieleze ni kwa namna gani kiongozi wa upinzani nchini humo, Alexei Navalny alipewa sumu ikiwa tayari Ujerumani imebaini ni kemikali aina ya Novichok.

Waziri Raab ameieleza kituo cha habari cha Sky News kwamba, jambo ambalo lipo wazi kwa sasa ni kwamba serikali ya Urusi ina maswali mengi magumu ya kujibu.

Amesema, iwapo tukio hilo lilihusisha Serikali au njia nyingine, Urusi ina jukumu la kuhakikisha kuwa silaha za kemikali hazitumiwi nchini humo.

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Heiko Maas amesema,Ujerumani itajadili suala la kuiwekea vikwazo Urusi kuhusiana na tukio la kumlisha sumu Alexai Navalny ikiwa Urusi haitotoa maelezo ya kina.

Navalny ambaye ni mwanaharakati wa kupinga ufisadi aliumwa mwezi uliopita na kutibiwa nchini Serberia kabla ya kukimbizwa mjini Berlin, Ujerumani.

Aidha, hivi karibuni Serikali ya Ujerumani ilieleza kuwa, kulikuwa na ushahidi wa wazi kuwa, mpinzani huyo wa Rais Vladmir Putin alipewa sumu aina ya Novichok.

Waziri Maas alilieleza gazeti la kila siku la Ujerumani Bild kwamba,wana matarajio makubwa kwa Serikali ya Urusi kutatua uhalifu huo ambao aliutaja ni mkubwa.

“Na ikiwa Serikali haihusiki na shambulio hilo, basi ni wajibu wake kusema ukweli,” Waziri huyo alinukuliwa na Gazeti la Bild.

Hata hivyo, Serikali ya Urusi imekana kuhusika na shambulio hilo na waziri wake wa Mambo ya Nje, Sergei Lavrov alisema, Ujerumani imeshindwa kutoa ushahidi wowote kwa waendesha mashitaka wa Moscow.

Aidha, Msemaji wa wizara hiyo, Maria Zakharova aliituhumu Ujerumani kwa kukwamisha juhudi za uchunguzi wa kesi ya Navalny.

“Berlin inazuia mchakato wa uchunguzi ambao imeuitisha. Kwa makusudi. Kama serikali ya Ujerumani inasema kweli kwenye taarifa zake basi itatakiwa kujibu kwa haraka maombi ya ofisi ya mwendesha mashitaka wa Urusi,”Msemaji huyo alieleza katika ukurasa wake wa Facebook.