Na Penina Malundo,TimesMajira
KATIKA uchumi wa taifa lolote, Serikali haiwezi kuangaliwa kwa ukubwa wa idadi ya watumishi, taasisi au kiasi cha fedha kinachotumia pekee, bali uangalia namna inavyokusanya na kutumia fedha za umma ipasavyo na namna inavyoshirikisha sekta binafsi kushiriki katika shughuli za kiuchumi.
Kwa Tanzania, mjadala kuhusu ukubwa wa Serikali unazidi kuwa muhimu kutokana na nafasi kubwa ya matumizi ya umma katika uchumi, huku kodi ikiwa miongoni mwa vyanzo vikuu vya mapato vinavyowezesha ukuaji wa Uchumi.
Matumizi ya Kodi mara nyingi katika nchi, Serikali kugharamia katika huduma za msingi kama elimu, afya, miundombinu, ulinzi na huduma nyingine za kijamii katika kuhakikisha maendeleo yanapatikana kwa haraka.
Tafiti mbalimbali zilizofanyika kuhusu mapato ya kodi katika nchi yanaweza kuwa kati ya asilimia 15 hadi 40 ya pato la taifa, huku tofauti hizo zikitegemea kiwango cha maendeleo ya nchi, ukubwa wa uchumi usio rasmi, uwezo wa ukusanyaji wa kodi na sera zinazotumika.
Kwa Tanzania,kuongeza mapato ya ndani kuna umuhimu mkubwa kwa sababu huiwezesha Serikali kutekeleza mipango ya maendeleo bila kutegemea kwa kiwango kikubwa mikopo au misaada kutoka nje.

Hata hivyo, pamoja na kuongeza mapato, wataalamu wanaonya kuwa Serikali inapaswa kuhakikisha mfumo wa kodi hauwi kikwazo kwa uwekezaji na ukuaji wa sekta binafsi.
Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Liberty Sparks,Evans Exaud anasema kuna umuhimu wa kuangalia serikali inaukubwa gani katika uchumi,inagharimu kiasi,inazalisha nini na jamii inapata thamani gani kutokana na rasilimali zinazotumika kuiendesha.
Anasema Serikali kuwa si lazima iwe mbaya na Serikali ndogo si lazima iwe serikali bora bali kinacopaswa kuangaliwa ni thamani,motisa ,ufanisi na utendaji wa taasisi.
Exaud anasema takwimu zinasema kuwa katika chambuzi zao za kihistoria wa utendaji wa Tanzania katika eneo la ukubwa wa Serikali kati ya mwaka 2000 na 2022 unaonyesha mwenendo unaostahili kuchunguzwa.
Anasema katika kipindi cha mwaka 2000 hadi 2014, alama ya Tanzania ilibaki katika kiwango cha takribani 6.5 hadi 7.5,huku kuanzia mwaka 2015 walishuhudia kushuka kwa alama hiyo na kufikia takribani 6.2 mwaka 2022 katika mfululizo wa kihistoria waliocambua kama taasisi.

“Takwimu za hivi karibuni zilizotolewa na Taasisi ya Fraser, zinazotumia takwimu za mwaka 2023, zinaipa Tanzania alama 5.87 kati ya 10 katika kipengele cha ukubwa wa Serikali, huku Tanzania ikiwa katika nafasi ya 125 kati ya maeneo 165,” anasema.
UKUAJI WA UCHUMI
Mhadhiri na mtafiti wa Chuo Kikuu cha Ardhi, Dkt. Rosemary Mnongya, ambaye ni mmoja wa wajumbe waliohusika katika uandaaji wa Ripoti ya Ukaguzi wa Uhuru wa Kiuchumi Nchini, anasema uhuru wa kiuchumi unahusishwa kwa karibu na kiwango ambaco watu binafsi ,kaya na wafanyabiasara wanaruhusiwa kufanya maamuzi katika sughuli zao za kiuchumi.
Anasema mjadala wa uhuru wa kiucumi haupaswi kuwa wa kucagua kati ya serikali na sekta binafsi bali kujenga mfumo ambao kila upande unafanya kile ambacho una uwezo mkuwa zaidi ya kufanya.
Aidha anasema katika uchumi wa taifa, kodi ni moja ya nguzo muhimu zinazoiwezesha Serikali kutekeleza majukumu yake, kuanzia kutoa huduma za msingi kwa wananchi hadi kujenga miundombinu na kuweka mazingira yanayowezesha uwekezaji wa sekta binafsi.
Hata hivyo, pamoja na umuhimu huo, suala la kiasi cha kodi kinachokusanywa na namna fedha hizo zinavyotumika ni moja ya sehemu muhimu ya mjadala kuhusu ukubwa wa Serikali na nafasi yake katika uchumi.”Kodi ina nafasi kubwa katika ukuaji wa uchumi kwa sababu huiwezesha Serikali kupata rasilimali za kugharamia maendeleo.
”Fedha zinazokusanywa kupitia kodi zinaweza kurejeshwa katika uchumi kupitia ujenzi wa barabara, shule, hospitali, miradi ya maji, nishati na huduma nyingine muhimu,”anasisitiza
Akizungumzia umuhimu wa Sekta Binafsi,Mtaalam wa Sera wa Policy Forum,Samwel Mkwatwa anasema Tanzania inaweza kuongeza ufanisi wa uchumi kwa kuipa sekta binafsi nafasi kubwa zaidi ya kushiriki katika shughuli za uzalishaji na utoaji wa huduma, huku Serikali ikijikita katika kusimamia sheria, sera na miongozo.
Anasema Serikali inapoingia moja kwa moja katika shughuli za kibiashara, inaweza kujikuta ikitoka katika jukumu lake la msingi la kusimamia mazingira ya biashara na badala yake kushindana na sekta binafsi.
Kwa mujibu wa Mkwatwa, uzoefu wa nchi zilizoendelea unaonyesha kuwa shughuli nyingi za kibiashara zinaendeshwa na sekta binafsi, jambo linaloipa Serikali nafasi ya kujikita katika usimamizi wa uchumi na ukusanyaji wa kodi.
“Serikali inapofanya biashara, uwezo na tija yake huwa ndogo ukilinganisha na kampuni binafsi. Sekta binafsi ikipewa nafasi, Serikali inaweza kukusanya kodi zaidi huku ikipunguza mzigo wa gharama za uendeshaji,” anasema.
Samweli anasema Tanzania ina mashirika mengi ya umma ambayo baadhi yake yamekuwa yakihitaji msaada wa Serikali ili kuendelea kufanya kazi, hali inayoongeza mzigo kwa fedha za umma.
Anaeleza kuwa ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zimekuwa zikionyesha changamoto katika utendaji wa baadhi ya mashirika hayo, ikiwamo kutokuwa na uwezo wa kuzalisha mapato ya kutosha kukidhi gharama za uendeshaji.
Kwa maoni yake, baadhi ya shughuli zinazofanywa na mashirika ya umma zinaweza kupewa wawekezaji na kampuni binafsi, huku Serikali ikibaki na jukumu la kuweka kanuni, kusimamia ushindani, kuhakikisha huduma zinatolewa kwa viwango vinavyokubalika na kuimarisha ukusanyaji wa kodi.

More Stories
HESLB yavunja rekodi, yakusanya bilioni 235.5/-
Viongozi wanawake watakiwa kuvunja vikwazo vya kimfumo
Rais Dkt,Samia mgeni rasmi kilele cha mbio za Mwenge kitaifa Rukwa