October 12, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

HESLB yavunja rekodi, yakusanya bilioni 235.5/-

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira

LICHA ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kuvunja rekodi ya makusanyo ya mikopo kwa kukusanya Sh bilioni 235.5 katika mwaka wa fedha 2025/2026, takribani Sh bilioni 800 bado zinadaiwa kwa wanufaika ambao hawajajitokeza kurejesha mikopo yao, hali inayozua maswali kuhusu uendelevu wa mfuko huo wakati mahitaji ya ufadhili yanapoongezeka.

Hayo yamebainishwa Jijini Dar es Salaam jana na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia wakati kikao kazi kati ya bodi hiyo na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH).

Amesema makusanyo ya mikopo iliyoiva katika mwaka wa fedha 2025/2026 yalifikia Sh bilioni 235.5 dhidi ya lengo la Sh bilioni 220, sawa na asilimia 107 ya lengo lililowekwa.

“Hiki ndicho kiwango cha juu zaidi cha makusanyo kuwahi kufikiwa na taasisi hiyo tangu ilipoanzishwa mafanikio haya yanaambatana na deni kubwa ambalo bado halijakusanywa”amesema

Amesema jumla ya Sh trilioni 1.91 zimekusanywa tangu mwaka wa fedha 2005/2006 hadi Juni 2026, kati ya Sh trilioni 2.77 za mikopo iliyofikia muda wa kurejeshwa, sawa na ufanisi wa asilimia 69.

Dkt Kiwia amekema hesabu hizo zinaacha takribani Sh bilioni 860 za mikopo iliyokomaa bila kukusanywa katika kipindi hicho, ingawa si kiasi chote kinachoweza kuchukuliwa kuwa kimekataa kulipwa, kwa kuwa maelezo hayo hayatoi mgawanyo wa madeni kulingana na hali yake.

Aidha, amekiri kuwa bado kuna wanufaika wanaodaiwa takribani Sh bilioni 800 ambao hawajajitokeza kurejesha mikopo yao, hususani wale wanaofanya shughuli zao katika sekta isiyo rasmi.

“Wakati changamoto ya urejeshaji ikiendelea, Serikali imeongeza fedha kwa ajili ya ufadhili wa wanafunzi”amesema

Kwa upande wa mwaka wa masomo 2026/2027, bajeti ya mikopo na ruzuku imefikia Sh trilioni 1.06, ikilinganishwa na Sh bilioni 916.7 zilizotengwa mwaka uliotangulia huku ongezeko hilo likiwa sawa na asilimia 15.6.

Akizungumzia upande wa wanufaika, amesema bajeti ya mwaka 2025/2026 ilinufaisha wanafunzi 289,932, huku bajeti ya mwaka huu ikitarajiwa kuwafikia wasiopungua 300,000.

“Hii ina maana kuwa ongezeko la idadi ya wanufaika wanaotarajiwa ni takribani asilimia 3.5, kiwango kilicho chini ya ongezeko la bajeti”amesema

Amesema tofauti hiyo haimaanishi moja kwa moja kuwa fedha zinatumika bila tija.

Inaweza pia kuhusishwa na gharama za ufadhili kwa kila mwanafunzi, mabadiliko ya aina ya ufadhili au mahitaji ya wanafunzi.

Amesema katika awamu ya kwanza ya upangaji wa mikopo na ruzuku kwa mwaka wa masomo 2026/2027, alisema HESLB ilipanga jumla ya wanafunzi 165,775 kunufaika na ufadhili wenye thamani ya Sh bilioni 535.7.

Kati yao, wanafunzi 74,769 wa mwaka wa kwanza wa shahada ya awali walipangiwa mikopo ya Sh bilioni 246.88, huku wanafunzi 8,538 wa stashahada wakipangiwa Sh bilioni 22.9.

Kwa upande wa wanafunzi wanaoendelea na masomo, 79,115 wa shahada ya awali walipangiwa mikopo ya Sh bilioni 252.4, huku wanafunzi 1,554 wa stashahada wakipangiwa Sh bilioni 3.8.

Amesema Takwimu hizo zinaonesha ukubwa wa fedha zinazopitia HESLB, lakini tathmini ya tija yake inahitaji pia kufuatilia idadi ya wanafunzi wanaokamilisha masomo, kupata ajira au kujiajiri na hatimaye kuanza kurejesha mikopo yao.

Amesema katika tathmini ya mpango mkakati uliopita, HESLB ilieleza kuwa asilimia 72 ya waombaji wa mikopo waliokuwa na sifa walipangiwa mikopo.

Dkt Kiwia amesema Takwimu hiyo ina maana kuwa, kwa mujibu wa kipimo hicho, takribani waombaji 28 kati ya kila 100 waliokuwa na sifa hawakupangiwa mikopo katika kipindi kilichotathminiwa.

Katika hatua nyingine amesema Katika kuongeza makusanyo, HESLB imeendelea kutumia mikakati mbalimbali, ikiwamo kampeni za Fichua na Kiduchu Fresh Tunasonga.

“Kampeni ya Kiduchu Fresh Tunasonga, iliyozinduliwa Aprili 2026, inalenga kuwawezesha wanufaika wenye kipato kidogo kuanza kurejesha mikopo kwa kiasi kinacholingana na uwezo wao”amesema

Amesema mikakati hiyo inalenga kuongeza wigo wa wanaorejesha, hasa katika sekta isiyo rasmi, ambako kuwafikia wanufaika na kufuatilia mapato yao kunaweza kuwa changamoto.