October 12, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Viongozi wanawake watakiwa kuvunja vikwazo vya kimfumo

Na Penina Malundo,TimesMajira

VIONGOZI wanawake nchini wametakiwa kuondoa vikwazo vya kimfumo, ubaguzi na unyanyasaji vinavyowazuia kudumu na kupanda katika nafasi za uongozi, huku taasisi za umma na binafsi zikihimizwa kuweka mifumo ya haki inayowawezesha wanawake kutumia uwezo wao kikamilifu.

Wito huo umetolewa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Riziki Pembe Juma ni
katika Kongamano la Sita la Wanawake katika Uongozi lililoandaliwa na Taasisi ya UONGOZI.

Amesema taasisi zinapaswa kuhakikisha uwazi na usawa katika uteuzi, tathmini ya utendaji na upandishaji vyeo, ili wanawake wapate fursa za kuongoza majukumu muhimu na kujiandaa kwa nafasi za juu zaidi.

Amesema baadhi ya changamoto zinazowakabili wanawake katika uongozi zinatokana na mifumo na taratibu za taasisi, tamaduni za sehemu za kazi, mitazamo ya kijamii pamoja na kutokuwepo kwa usawa katika upatikanaji wa fursa na rasilimali.

Kwa mujibu wa Juma, hali hiyo inahitaji taasisi kuweka na kusimamia taratibu za kuzuia na kushughulikia ubaguzi na unyanyasaji mahali pa kazi, ili wanawake waweze kutekeleza majukumu yao kwa kujiamini na ufanisi.

Amesema umuhimu wa kuimarisha ushiriki wa wanawake katika uongozi unaungwa mkono na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inasisitiza usawa wa kijinsia, uwezeshaji wa wanawake na maamuzi shirikishi yanayowapa nafasi wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Ameongeza kuwa Mpango wa Muda Mrefu wa Utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 umeweka shabaha ya kufikia uwakilishi wa wanawake wa asilimia 50 katika nafasi za uongozi, hatua inayohitaji kuwekeza katika maarifa, ujuzi na vipaji vya wanawake ili kuongeza uwezo wao wa kushika majukumu makubwa zaidi.

Hata hivyo, amesema bado kuna pengo la uwakilishi wa wanawake katika nafasi za maamuzi duniani, akibainisha kuwa takwimu za Umoja wa Mabunge Duniani na UN Women zinaonyesha wanawake walikuwa na asilimia 27.5 ya viti vya ubunge duniani kufikia Januari 1, 2026.

Amesema takwimu hizo zinaonesha umuhimu wa kuendelea kuimarisha mikakati ya kuwawezesha wanawake kupata nafasi za uongozi na kuweka mifumo inayowasaidia kudumu na kukua katika nafasi hizo.

Naye Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Kadari Singo amesema taasisi hiyo inaendelea kutoa programu mbalimbali za mafunzo zinazolenga kuwajengea uwezo viongozi na wataalamu katika sekta tofauti, ikiwemo wanawake walio katika nafasi za uongozi.

Singo amefafanua kuwa taasisi hiyo inaendesha programu nne kuu za mafunzo ya uongozi ambazo ni Stashahada ya Uzamili ya Uongozi (Postgraduate Diploma in Leadership), inayodumu kwa mwaka mmoja, programu ya Wanawake katika Uongozi (Women in Leadership), Cheti cha Uongozi (Certificate in Leadership) na programu ya Kuandaa Viongozi (Making Leaders Program).

Ameeleza kuwa programu hizo zimekuwa sehemu ya juhudi za taasisi hiyo za kuimarisha uwezo wa viongozi, kuwapa maarifa ya kukabiliana na changamoto za uongozi na kukuza ujuzi wa kitaaluma.

Aidha, amewashukuru washirika na wafadhili wanaoiwezesha taasisi hiyo kutekeleza majukumu yake, akiwataja Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Umoja wa Ulaya (EU) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake (UN Women).

Amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kuendeleza mafunzo na programu zinazolenga kujenga viongozi wenye uwezo wa kuleta mabadiliko chanya katika jamii na taasisi wanazoziongoza.